Esther Musila afichua wakati alipokutana na mumewe wa kwanza, baba wa watoto wake

Mume wa kwanza wa Esther Musila, Bw Erick ambaye alipata naye watoto wake watatu aliaga dunia mwaka wa 2016.

Muhtasari

•Esther Musila amefichua kwamba alikutana na baba wa watoto wake wakati alipohamia jijini Nairobi kutoka Nakuru kwa ajili ya kazi. 

•Bintiye Musila, Gilda Naibei alisema walimpenda sana baba yao marehemu huku akieleza kuwa wakati Guardian Angel alipojiunga na familia alielewa kuwa hawakuhitaji baba mwingine.

Image: INSTAGRAM// ESTHER MUSILA

Mke wa mwanamuziki Guardian Angel, Esther Musila amefichua kwamba alikutana na baba wa watoto wake wakati alipohamia jijini Nairobi kutoka Nakuru kwa ajili ya kazi. 

Katika mahojiano na KTN, mama huyo wa watoto watatu alifichua kuwa alipata kazi katika kampuni moja iliyokuwa karibu na ikulu ya Nairobi na ni wakati akiwa katika kazi hiyo ambapo alianza kujenga maisha yake. Alisema alipata kazi hiyo kwa kuiomba baada ya kupata anwani ya kampuni iliyomuajiri kwenye orodha ya simu. 

Baada ya kukutana na mumewe huyo wa zamani, malkia huyo mwenye umri wa miaka 53 alianzisha familia naye na walijaliwa watoto watatu pamoja.

“Nilikaa na rafiki yangu niliyekuwa naye Kianda kwa takriban mwezi mmoja nikiwa natafuta mahali pa kuishi, maisha yakaanza. Wakati huo, ndipo nilipokutana na babake Gilda na kisha tukaanzisha familia. Nilipata watoto wangu watatu naye kisha nikachoka na kazi hiyo,” Bi Esther Musila alisimulia. 

Baada ya kugura kazi hiyo yake ya kwanza jijini Nairobi, mama huyo wa watoto watatu aliomba kazi nyingine katika benki wakati akiwa na ujauzito wa mtoto wake wa kwanza.

Katika mahojiano hayo, alifunguka jinsi alivyowasilisha mkojo wa mama yake kwa vipimo vya ujauzito kabla ya kupata kazi hiyo kwani lilikuwa ni hitaji la benki kwa wanawake kupimwa ujauzito kabla ya kuajiriwa.

“Mama alinipa mkojo wake. Nilijua nina mimba. Nilihitaji kwenda kwenye mahojiano ya kazi. Nilisafiri na mkojo wa mama yangu kutoka Nakuru hadi Nairobi,” Esther Musila alisema.

Kwa bahati alipata kazi hiyo baada ya kuwasilisha mkojo wa mama yake na alihudumu katika benki hiyo kwa takriban miaka 6 kabla ya kujiuzulu ili kuwatunza watoto wake ambao walikuwa wadogo sana wakati huo.

Mume wa kwanza wa Bi Esther Musila, Bw Erick ambaye alipata naye watoto wake watatu aliaga dunia mwaka wa 2016.

Katika mahojiano ya awali, bintiye Musila, Gilda Naibei alisema walimpenda sana baba yao marehemu huku akieleza kuwa wakati Guardian Angel alipojiunga na familia alielewa kuwa hawakuhitaji baba mwingine.

"Tulikuwa na baba, tuko na baba. Alikuwa anaitwa Erick, roho yake ipumzike kwa amani. Alikuwa baba mzuri, tulimpenda. Tulimpoteza 2016. Naweza sema niko na baba. Guardian sana sana ni kama mshauri" Gilda alisema.