Ex wa Karen Nyamu amsifu Samidoh, azungumzia kupewa upendeleo wa kimapenzi na seneta huyo

DJ Saint Kevin ambaye ni baba wa mtoto wa kwanza wa Karen Nyamu alimtaja Samidoh kuwa mtu mzuri.

Muhtasari

•DJ Saint Kevin alikanusha kupata upendeleo wowote wa kimapenzi kutoka kwa mpenzi huyo wake wa zamani.

•Pia alitakiwa kujibu kuhusu uhusiano wake wa sasa na Bi Nyamu ambapo alifichua kuwa wanashirikiana vyema katika uzazi.

Karen Nyamu na mzazi mwenzake DJ Saint Kevin
Image: HISANI

Mzazi mwenza wa Karen Nyamu, DJ Saint Kevin amefichua kwamba amewahi kukutana na mpenzi wa sasa wa seneta huyo wa kuteuliuwa, Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, Kevin ambaye ni baba wa mtoto wa kwanza wa mwanasiasa huyo alimtaja staa huyo wa Mugithi kuwa mtu mzuri.

"Nimekutana na yule jamaa, ni mtu mzuri sana. Hakuna uhusiano mbaya," DJ Saint Kevin alisema.

Akizungumzia hisia zake kuhusu Karen Nyamu kuwa katika uhusiano mpya, deejay huyo alisema, "Jamaa huyo (Samidoh) alikuja baadaye sana, kila mtu anaruhusiwa kuendelea."

Mtumbuizaji huyo pia alitakiwa kujibu kuhusu uhusiano wake wa sasa na Bi Nyamu ambapo alifichua kuwa wanashirikiana vyema katika uzazi.

“Yeye ni mtu mzuri; yeye ni mama mzuri kwa mtoto wetu. Sisi tunashirikiana katika malezi. Hakuna damu mbaya, sisi ni wazazi wenza,” alisema.

Aliongeza, “Tunaishi maisha tofauti kabisa, yeye ana maisha na mimi nina yangu, na niko poa nayo. Tunakutana katikati linapokuja suala la watoto, hiyo ni kama wakati pekee tunakutana."

Saint Kevin pia alikanusha kupata upendeleo wowote wa kimapenzi kutoka kwa mpenzi huyo wake wa zamani akisema, "Hakuna marupurupu, mimi huenda kumchukua mtoto kila wiki na tuko vizuri. Kisha ninamrudisha, na ndivyo hivyo."

DJ Saint ndiye baba wa mtoto wa kwanza wa Karen Nyamu. Wawili hao walichumbiana kwa kipindi kabla ya kwenda njia tofauti.

Mwaka jana, mcheza santuri huyo alizungumza kuhusu jinsi mahusiano yao ya miaka kadhaa yalivyokuwa sumu.

Akiongea kwenye ukurasa wake wa Instagram,  alisema kuwa kazi yake kama DJ ilichangia uhusiano wao mbaya.

“Kama Dj huwa natangamana na wanawake mara kwa mara, shabiki wa kike anaweza kupanda jukwaani na kukupa busu shingoni huku akiomba wimbo na Karen alishindwa kuvumilia. Hata kama hatasababisha drama kwenye hafla hiyo, tunapoingia kwenye gari kurudi nyumbani, ni msomo mpaka nyumbani," alifichua.

DJ Saint aliongeza kuwa walizozana kila siku na kusababisha mvutano ambao ulisababisha kutengana kwao.

"Ilikuwa ni vita baada ya vita, na mimi kuamua kuondoka tulikuwa tumefikia hatua ya kutorudi nyuma. Kila mara ilikuwa mabishano na niliona sio sawa kwa sisi kumlea mtoto wetu katika mazingira hayo. Niliamu kumpa nafasi na ikawa sawa. Ilikuwa ni sumu, kila siku mapigano," Dj Saint aliendelea kusimulia.

Alisema kwamba Karen ni mama mzuri na akabainisha kuwa wanashirikiana vizuri katika malezi ya binti yao.