"Gym na diet siwezi!" Paula amsihi Marioo kupunguza mahaba anayompa kwa hofu ya kunenepa

Paula alidokeza kuwa mahaba mazito ambayo Marioo amekuwa akimuogesha nayo yanampa raha tele maishani.

Muhtasari

•Paula amemtaka Marioo kupunguza mapenzi anayompa huku akidai kuwa furaha inayotokana nayo inamfanya azidi kuwa mnene.

•Kajala alikiri upendo wake mkubwa kwa mkwe huyo wake huku akimtambua  kama mwanawe wa pekee.

Paula na mpenzi wake Marioo
Image: HISANI

Mwanamitindo Paula Kajala ameendelea kujivunia mahusiano yake na  mwimbaji Omari Mwanga almaarufu Marioo yanayoonekana kuwa kamilifu.

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu jioni, binti huyo wa pekee wa muigizaji Kajala Masanja mwenye umri wa miaka 21 alidokeza kuwa mahaba mazito ambayo Marioo amekuwa akimuogesha nayo yanampa raha tele maishani.

Kufuatia hali hiyo, Paula sasa kwa utani amemtaka mwimbaji huyo wa kibao ‘Mi Amor’ kupunguza mapenzi ambayo amekuwa akimpa huku akidai kuwa furaha inayotokana nayo inamfanya azidi kuwa mnene.

"Omary Ally Mwanga!! Punguza hizi raha unazonipa bana, mi nanenepa alafu gym na diet siwezi mwenzio," Paula Kajala alisema.

Wapenzi hao wamekuwa wakichumbiana kwa miezi kadhaa iliyopita tangu walipoweka wazi mahusiano yao mwezi Aprili. Marioo anaonekana kuwa na uhusiano mzuri, si tu na Paula bali pia na mama mkwe wake Kajala Masanja.

Jumatatu asubuhi, Kajala alikiri upendo wake mkubwa kwa mkwe huyo wake huku akimtambua  kama mwanawe wa pekee.

“Ni mwana pekee niliye naye ,@marioo_tz makopa mengi sana kwako,” Kajala aliandika na kuambatanisha na emoji za moyo zinazoashiria upendo.

Ujumbe wa Kajala uliandamana na picha ya mwimbaji huyo wa kibao 'Mi Amor'.

Siku ya Jumamosi jioni, Kajala alifanya karamu kubwa ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa ambapo Marioo alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa waliopamba hafla hiyo. Muigizaji huyo alisherehekea siku yake maalum kwa mtindo huku akitimiza miaka 40.

Marioo alitumia hafla hiyo kummiminia upendo mama mkwe wake na kumthamini kwa kumpa binti yake.

“Upendo ambao naupata kutoka kwa mama mkwe ni mkubwa sana. Tushaongea vitu vingi mimi na mama yangu, tumeshapanga vitu vingi sana. Mimi niseme tu nampenda sana na Mungu amfanyie upesi mambo yazidi kuwa mazuri,” Marioo alisema mbele ya wageni waliokuwa wamejumuika kwa karamu hiyo.

Aliongeza, “Nafurahi kwamba kanikabidhi mtoto, sio rasmi lakini. Nimefurahi, nashukuru nampenda sana mama yangu. Mungu akubariki.”

Baada ya hotuba yake, Marioo alifikia begi lililojaa pesa ambazo alikusudia kumpa mpenzi huyo wa zamani wa bosi wa Kondegang Harmonize kama zawadi ya siku ya kuzaliwa.

Kabla ya kupokea pesa hizo, Kajala alifunguka kuhusu uhusiano mzuri kati yake na mkwe wake Marioo.

Alimtambua mwimbaji huyo kama mwanawe na akafichua kuwa wanafanya mipango mikubwa pamoja.

“Omari ni kijana wangu. Tuko poa sana, tunaingia vizuri mno. Tunaongea vitu vingi sana, ata asiponipa mimi chochote hapa, niko poa kwa sababu kuna vitu vingi sana tunafanya nyuma ya pazia nyinyi hata hamjui. Uwepo wake hapa ni mkubwa mnachotaka atoe kwenye sahani. Shukran kwa kuja,” Kajala alisema.

Baada ya kusifiwa, Marioo aliendelea kumuogesha mama huyo wa mpenzi wake noti za pesa kiasi ambacho hakikujulikana.

Paula alitangaza mahusiano yake na Marioo  Aprili, muda mfupi baada ya aliyekuwa mpenziwe, Rayvanny kurudiana na Fahyma.