Harmonize aacha pombe baada ya kulewa na kuropokwa kuhusu ex wake, Kajala

Konde Boy ametangaza kuwa hatawahi kukata maji tena.

Muhtasari

•Katika taarifa fupi siku  ya Jumanne, staa huyo wa bongo fleva alimwomba Mungu amsaidie anapoanza maisha bila pombe.

•Tangazo hilo linakuja siku chache tu baada ya Harmonize kubugia mvinyo na kulewa kisha kuropoka kuhusu Kajala.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Bosi wa Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ametangaza kuwa hatawahi kukata maji tena. 

Katika taarifa fupi siku  ya Jumanne, staa huyo wa bongo fleva alimwomba Mungu amsaidie anapoanza maisha bila pombe.

“Natangaza rasmii nimeacha pombe. Sinywii tenaa. Maisha Mungu Nisimamie,” Harmonize alisema kwenye Instagram.

Tangazo hilo linakuja siku chache tu baada ya mwimbaji huyo wa kibao ‘Single Again’ kubugia mvinyo na kulewa kisha kuropoka kuhusu aliyekuwa mpenzi wake, muigizaji Fridah Kajala Masanja kwenye Instagram.

Mapema mwezi huu, Konde Boy alitishia kufunguka kuhusu utapeli wa Kajala baada ya kubugia chupa kadhaa za tembo na kulewa.

Siku ya Jumatano wiki iliyopita, mara baada ya mahojiano ya Kajala na wanahabari, Harmonize alitangaza kuwa yuko tayari kulewa na hata akaendelea kukata maji.

“Ohooo!!! Pombe zimeanza kuingia,” Harmonize alitangaza katika moja ya taarifa zake kwenye mtandao wa Instagram.

Katika sasisho lingine, alidokeza kuwa tayari alikuwa amelewa.

"Alooo nimelewa!!!"

Siku iliyofuata, Alhamisi, mwanamuziki huyo aliandika taarifa ndefu ambapo alimshambulia Kajala na kumtaka aache kugombana naye kwenye mitandao ya kijamii na badala yake atafute mwanaume wa kumuoa.

Harmonize alidokeza kuwa haijulikani ni kwa nini mama huyo wa binti mmoja bado hajaolewa licha ya umri wake mkubwa.

“Tafuta bwana mzee mwenzio hata mganga kienyeji aliyezeeka zeheka. Acha kubishana na watoto online na kujitia moyo!! Usikute anajua anaweza kukutana na bang la take me back tena!! Kinachomfanya asiolewe hatukijuwi, kazi ni kumfwata fwata binti tuu!! Ukweli unaujua wewe!!” Harmonize alifoka siku ya Alhamisi asubuhi.

Staa huyo alidai kuwa Kajala amekuwa akifika kwake katika jaribio la kuomba msamaha ila walinzi wamekuwa wakimtimua.

Alimtajia muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 baadhi ya mali yake yakiwemo magari 10 na kubainisha kuwa mama yake na binti yake Zulekha Rajabu wangerithi mali yote anayomiliki iwapo angefariki leo.

“Kama unahisi sijamove on ni tatizo lako la uzee pia!! Sikukugombeza, sikukutukana. Nilikudharau na ndio maana umekuwa ukisema ukisema akimzoea mtu anamdharau. Hakuna aliyekuwa akijua hili hata watu wa karibu ndio maana kila mtu alikuwa anadhani nimecheat na sijui amelowa girl lol,” Harmonize alimwandikia ex huyo wake.

Konde Boy alimwita mpenziwe huyo wa zamani 'mwizi' na akamweleza bayana kuwa hafikii hata robo ya sifa za mpenzi wake wa sasa.

Mwimbaji huyo wa wimbo wa ‘Single Again’ alifoka baada ya kudokeza kuwa alikuwa amebugia tembo na kulewa. Hapo awali, alikuwa ameahidi kufunguka kuhusu uhusiano wake na Kajala uliovunjika baada ya kulewa.

“Niliwaambia nitalewa,” alisema huku akimalizia kutoa taarifa yake.