"Hiyo ni noma!" Ngesh amvunja moyo Stevo Simple Boy baada ya kumtongoza awe mpenzi wake

Ngesh alibainisha kuwa tayari yuko kwenye mahusiano thabiti na mwanamume mwingine.

Muhtasari

•Stevo alikiri mapenzi yake mazito kwa Ngesh na akamuomba awe mchumba wake ikiwa hayuko kwenye mahusiano kwa sasa.

•Katika mahojiano, Ngesh hata hivyo alikataa ombi la Stevo Simple Boy na kuweka wazi kwamba hamtaki.

amemkataa Stevo Simple Boy
Ngesh amemkataa Stevo Simple Boy
Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki chipukizi wa Kenya Mary Wangeci almaarufu Ngesh wa Vasha amekataa waziwazi ombi la rapa Stevo Simple Boy la kuwa mpenzi wake.

Stevo alikuwa ametengeneza klipu ya video ambayo alitumia kukikiri mapenzi yake mazito kwa mwimbaji huyo mwenzake na akaendelea kumwomba awe mchumba wake ikiwa hayuko kwenye mahusiano kwa sasa.

Mwimbaji huyo wa kibao ‘Mihadarati’ aliwaomba Wakenya wamsaidie kufikisha ombi lake tamu kwa Ngesh ili kuushinda moyo wake.

“Huyu ni Stevo Simple Boy, Mondi wa Kenya maze. Kuna mwanadada pale nimeona amenivutia sana, anaitwa Kaveve Kazoze. Kama ako single, mwambie Stevo Simple Boy, mzee wa matulinga namtamani,” Stevo alisema kwenye video hiyo.

“Mfikishieni ripoti mwambie Stevo Simple Boy nimeleta kwake, wangu lazizi, wangu habibi, kwake sitamsuta nitakuwa nay eye au sio na mambo yako freshi. Aje na awe mchumba wangu, na mambo iwe freshi,” aliongeza kabla ya kutuma busu moto kwa msanii huyo wa kundi la Spider Clan.

Katika mahojiano ya simu na kituo cha redio cha humu nchini, Ngesh hata hivyo alikataa ombi la Stevo Simple Boy na kuweka wazi kwamba hamtaki.

Muimbaji huyo wa kibao ‘Kaveve Kazoze’ alibainisha kuwa bado alikuwa hajaitazama video ambayo Stevo aliitengeneza na kueleza kuwa ni marafiki zake ambao walimtumia picha kumfahamisha kuhusu ombi la rapa huyo.

“Sijona video, nimeona mapicha tu natumiwa mimi sijaona video. Mimi namtaka aje sasa? Mimi nasema ata video sijaona, Achana na yeye,” Ngesh alisema.

Malkia huyo wa muziki kutoka kaunti ya Nyandarua alifichua kuwa tayari yuko kwenye mahusiano thabiti na mwanamume asiyetambulishwa na akadokeza kuwa hana nia ya kutafuta mwanamume mwingine.

“Mimi niko na mtu. Hiyo ni noma. Mimi sikuwangi na 2nd thought. Usijali mpenzi wangu anaitwa,” alisema Ngesh.

Katika mahojiano ya mwezi uliopita, Ngesh alikiri kuwa yuko kwenye mahusiano na mwanamume ambaye anaishi nyumbani kwao, Naivasha.

“Mimi niko na mtu. Nadate. Ako Naivasha,” Ngesh alisema.

Aidha, mwanamuziki huyo chipukizi alikanusha tetesi za kuwa mwanachama wa LGBTQ ambazo zilikuwa zikienezwa.

Ngesh alibainisha kwamba hata hajui herufi LGBTQ zinasimamia nini.

“Mimi siwezi kuwa na nini kama hizo. Mimi ata sijui maana ya herufi hizo,” Ngesh alisema.

Mwimbaji huyo wa 'Kaveve Kazoze’ pia aliweka wazihakuna mwanamke yeyote amechukua hatua ya kumtongoza kwa nia ya kuchumbiana naye, kinyume na tetesi ambazo zimekuwa mjini. Tangu alipopata umaarufu, kumekuwa na tetesi kwamba Ngesh huenda ni msagaji kwa kuzingatia mtindo wake wa mavazi na mwonekano wake.