Kajala ajibu madai ya Harmonize kuwa amekonda baada ya kuachana naye, aliuza Range Rover

Kajala alisema hakufadhaishwa na kuvunjika kwa mahusiano yake na Harmonize kwa kuwa sio mwanamume wa kwanza kuwa naye maishani.

Muhtasari

•Kajala alidokeza kuwa kupungua kwa ukubwa wa mwili wake ni kutokana na mazoezi mengi ambayo amekuwa akifanya.

•Kajala alikanusha madai kuwa tayari ameshauza gari aina ya Range Rover aliyomnunulia staa huyo wa bongo fleva.

amejibu madai ya Harmonize.
Kajala amejibu madai ya Harmonize.
Image: HISANI

Muigizaji mkongwe wa filamu bongo, Fridah Kajala Masanja hatimaye amevunja ukimya baada ya aliyekuwa mpenzi wake Harmonize kuibua madai mazito dhidi yake.

Miongoni mwa madai ya bosi huyo wa Konde Music Worldwide dhidi ya Kajala ni kwamba muigizaji huyo anaonekana kuwa na msongo wa mawazo na kwamba kwa kweli amepungua baada ya kutengana naye mwaka jana.

Huku akijibu madai hayo wakati wa kikao na wanahabari siku ya Jumatano, mama huyo wa binti mmoja alidokeza kuwa kupungua kwa ukubwa wa mwili wake ni kutokana na mazoezi mengi ambayo amekuwa akifanya

“Mimi sioni kama nimetikisa. Mimi najua nafanya mazoezi ndio maana niko hivi,” Kajala alisema.

Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 aliweka wazi kwamba hakufadhaishwa hata kidogo na kuvunjika kwa mahusiano yake na Harmonize kwa kuwa sio mwanamume wa kwanza kuwa naye maishani.

Kajala pia alikanusha madai kuwa tayari ameshauza gari aina ya Range Rover aliyomnunulia staa huyo wa bongo fleva wakati alipokuwa akimuomba msamaha mapema mwaka jana akilenga kufufua mahusiano yao ambayo yalikuwa yamevunjika mwaka  wa 2021.

“Range sijaiuza, Range ipo. Kuhusu kutumia Toyota, ni kweli mara nyingi natumia gari la Paula. Huwa nahisi inakuwanga very comfortable kwa sababu lile (Range) likiwa na jina kuna sehemu huwa nataka kwenda na sitaki kuitwa Kajala. Kwa hiyo mara nyingi natumia gari la Paula. Hata ni kutumia Toyota ama ST, ni gari,” alisema.

Kuhusu kuwa na nambarisiri za akaunti zote za benki za mwanamuziki huyo, Kajala alibainisha kuwa kila mtu katika Kondegang anazo kwani mwimbaji huyo wa kibao ‘Single Again’ huwa anamtuma yeyote kwenda kununua au kupata kitu kwa kutumia kadi zake za mkopo.

Pia alijibu kuhusu kupokea 10% ya mapato ya staa huyo wa bongo kutokana na shoo na dili zote alizofanya ambapo aliweka wazi kwamba alipata kitu katika miezi miwili ya mwisho ya mahusiano yao.

“Tulivyokuwa tunaanza, ilikuwa sio kweli. Alafu miezi miwili kabla ya mimi na yeye kuachana ndio alinipea hiyo asilimia kumi. Alafu tutakuja tukaachana. Kama yeye alisema ni asilimia kumi, basi ni asilimia kumi,” alisema Kajala.

Wiki iliyopita, Harmonize na Kajala walishambuliana mitandaoni baada ya mwimbaji huyo kuachia wimbo ‘Dear Ex’ ambapo alifunguka baadhi ya masaibu ambayo aliwahi kupitia na mama huyo wa Paula Kajala. Harmonize alifichua mambo mengi kuhusu Kajala lakini muigizaji huyo alitoa majibu ya kimafumbo tu.