Karen Nyamu afunguka kwa nini DP Gachagua alimtishia Samidoh kufuatia mzozo uliotokea Dubai

DP Gachagua alimtaka Samidoh kuwadhibiti wapenzi wake na akatishia kumkataza kusafiri nje ya nchi iwapo angeshindwa.

Muhtasari

•Karen Nyamu alifunguka kuhusu uhusiano wao wa karibu na DP Gachagua na jukumu kubwa ambalo anacheza maishani mwao.

•Mwezi Januari, Gachagua alimwambia Samidoh kuchukua udhibiti wa mahusiano yake na kuzuia mizozo iliyokuwa ikishuhudiwa.

DP Rigathi Gachagua, Samidoh, Karen Nyamu
Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amefichua kwa nini naibu rais Rigathi Gachagua alimzomea hadharani mpenzi wake Samuel Muchoki kufuatia ugomvi uliomhusisha yeye, mwimbaji huyo na mkewe Edday Nderitu jijini Dubai mwezi Desemba.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na Ala C kwenye kipindi cha Reke Ciume na Ene, mama huyo wa watoto watatu alifunguka kuhusu uhusiano wa karibu kati yao na kiongozi huyo wa pili katika utawala wa nchi na jukumu kubwa ambalo anacheza maishani mwao.

Nyamu alisema DP Gachagua ni kama baba kwake na Samidoh na mara nyingi huwa anawapa ushauri, kama anavyofanya kwa vijana wengine wengi.

“Naibu rais ni mtu rahisi, ni rafiki yetu. Anawashauri vijana, kwetu sisi ni kama baba,” Nyamu alisema.

Aliongeza, “Nyinyi nyote mnaweza kumuona kama naibu wa rais lakini kwetu sisi tunamwona kama baba. Kamwe hana matatizo, ni mtu wa kushauri watu wengi. Aliongea kwa sababu mambo yetu yako wazi."

Seneta huyo wa UDA alidokeza kuwa yeye na mpenziwe Samidoh wanamheshimu naibu rais na kila mara huwa wanasikiliza ushauri wake mzuri.

Mapema mwaka huu, DP Rigathi Gachagua alimwambia Samidoh kuchukua udhibiti wa mahusiano yake na kuzuia mizozo iliyokuwa ikishuhudiwa huku akitishia kumzuia kusafiri nje ya nchi iwapo angeshindwa.

Gachagua alikuwa akirejelea drama iliyotokea kati ya mwimbaji huyo wa Mugithi, mkewe Edday Nderitu na mpenzi wake Karen Nyamu jijini Dubai. Alibainisha kuwa Samidoh amepata heshima ya wengi kupitia nyimbo zake na sasa anapaswa kurejesha utulivu katika familia yake na kuhakikisha adabu inatawala.

"Sasa wewe Samidoh ucontrol watu wako. Panga panga hiyo maneno yako na ukishindwa, tutakukataza kwenda ng'ambo," alisema Gachagua kwa mzaha.

Alisema mwimbaji huyo anapotoka kwenda kutumbuiza katika nchi ya kigeni, anapaswa kukumbuka kuwa nchi nyingi za kigeni hazithamini ndoa za wake wengi.

Gachagua alikuwa akizungumza wakati wa ibada ya mazishi ya dadake Waziri wa Biashara Moses Kuria Pauline Nyokabi. Samidoh pia alikuwepo.

Mwezi Desemba mwaka jana, video ilisambaa mtandaoni ikimuonyesha Nyamu na mke wa Samido Edday wakipigana vibaya kwenye tamasha jijini Dubai ambapo Samidoh alikuwa akitumbuiza.

Mzozo kati ya wawili hao ulishuhudia Nyamu akitolewa kwa nguvu kutoka kwa jukwaa na kufukuzwa na mlinzi.

Katika klipu tofauti, Nyamu alirekodiwa akicheza jukwaani huku Samidoh na mwimbaji wa nyimbo za injili Karangu Muraya wakitumbuiza.

Wakati huo ndipo seneta huyo wa kuteuliwa alipofukuzwa baada ya ugomvi mwingine kutokea.

Wakili huyo baadaye alilaumu matendo yake kwa pombe, tabia ambayo aliapa kuacha kuanzia Januari mwaka huu.