Kwa nini mzozo wa Akothee na dadake mdogo Cebbie Koks bado haujaisha

"Sitarudiana na wewe ikiwa hautaniambia nilikukosea wapi kwa sababu naweza kuishia kufanya kosa lile lile," Akothee alisema.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watano alidai kuwa bado haelewi jinsi alivyomkosea mdogo wake hadi mzozo kuanza kati yao.

•Alibainisha kuna haja ya jambo lililozua migogoro kuzungumziwa na kusuluhishwa kabla ya wao kupiga hatua ya maridhiano.

katika picha ya maktaba.
Cebbie Koks na dadake mkubwa Akothee katika picha ya maktaba.
Image: INSTAGRAM//

Mwimbaji na mjasiriamali maarufu wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amedokeza kuwa bado uhusiano mzuri kati yake na dadake mdogo Cebbie Koks Nyasego haujarudi.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na gazeti la The Nairobian, mama huyo wa watoto watano alidai kuwa bado haelewi jinsi alivyomkosea mdogo wake hadi mzozo kuanza kati yao.

Alibainisha kuwa kuna haja ya jambo lililozua migogoro kuzungumziwa na kusuluhishwa kabla ya wao kupiga hatua hiyo nyingine ya maridhiano.

"Hiyo ni familia yangu na msamaha haimaanishi kupatana. Sitarudiana na wewe ikiwa hautaniambia nilikukosea wapi kwa sababu naweza kuishia kufanya kosa lile lile. Ikiwa tutasameheana kwa sababu ya uhusiano wa kihisia na familia, basi tutaumizana zaidi,” Akothee alisema.

Msanii huyo ambaye maisha yake yamezungukwa na drama nyingi aliendelea kulalamika kuhusu masaibu yanayompata kutokana na hadhi yake na hali yake.

 “Kwa hiyo, bora tushughulike na tembo aliye chumbani na kusema unajua nini, nilikosea. Ninaadhibiwa kwa kuwa mtu maarufu na kuwa na utu. Siku zote niliambiwa wewe ni mtu mkubwa, dada mkubwa,” aliongeza.

Akothee hata hivyo alithibitisha upendo wake mkubwa kwa familia yake, lakini akasisitiza haja ya kuweka mipaka kati yao ili kulindana.

Mama wa watoto watano na dadake mdogo Cebbie Koks ambaye jina lake halisi ni Elseba Awuor Kokeyo wamejulikana kuzozana kwa muda sasa.

Katikati mwa mwaka jana, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alikiri kwamba kuna mgawanyiko mkubwa katika familia yake.

Akizungumza katika mahojiano na Presenter Ali,  aliwashutumu ndugu zake kwa kutosimama naye licha ya kuwa amewasaidia wote.

‘Nimesaidia familia yangu.Nilipopata umaarufu, familia yangu haikuwahi kujua mahali nilipokuwa na nilichokuwa nikifanya. Baada ya hapo niliwasaidia wote. Nikichapisha taarifa zangu za benki leo, mtagundua wanafamilia wangu wote wametabasamu hadi benki,” alisema.

Mwimbaji huyo alimshutumu dada yake mdogo Cebbie Koks kwa kuwashawishi wanafamilia wengine dhidi yake.

Alidai kwamba kaka zake hawakuichukulia kwa uzito harusi yake iliyofanyika Aprili kwani Cebbie alidaiwa kuwashawishi wanafamilia wengine kwamba ilikuwa njama ya kuharibu harusi yake na wakili Steve Ogolla ambayo ilifanyika mwezi Desemba.Alisema kisa hicho kilimfanya aanze kujitenga na familia yake na kufikiria kuishi maisha yake mbali nao.

"Polepole nilianza kujitenga, nikijitambua mimi ni nani. Katika luo huwa wanakungoja siku ukifa, nilituma mtu kuwaambia familia yangu kuwa mimi ni mtu wa serikali, Nikifa leo serikali itanizika. Mimi si mtu mwingine yeyote tu. Mazishi yangu yatakuwa makubwa kuliko harusi yangu, wasiwe na wasiwasi kuhusu mimi kurudi kwao,” alisema.

Hata hivyo aliweka wazi kuwa ana uhusiano mzuri na babake ambaye alimtaja kama shabiki wake mkubwa.