Mamake Diamond ajawa bashasha baada ya kuzawadiwa pesa, kupigwa busu na mkwe wake Zuchu

Mtunzi huyo wa kibao ‘Sukari’ alimbusu Mama Dangote na kumkumbatia huku akimtakia heri ya siku ya kuzaliwa.

Muhtasari

•Mama Dangote alionekana akiwa amejawa na tabasamu usoni mwake huku akimwagiwa pesa na mwanamuziki huyo wa WCB.

•Wawili hao walionekana kuwa na wakati mzuri pamoja na kufurahiya sana huku hayo yote yakifanyika.

Image: INSTAGRAM// MAMA DANGOTE

Siku ya Jumanne jioni, mamake bosi wa WCB Diamond Platnumz, Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote alionyesha noti za pesa alizozawadiwa na malkia wa bongofleva Zuhura Othman almaarufu Zuchu.

Katika video ambayo pia alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, Mama Dangote alionekana akiwa amejawa na tabasamu usoni mwake huku akimwagiwa pesa na mwanamuziki huyo ambaye kwa muda mrefu amekuwa akidaiwa kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanaye Diamond. 

Zuchu alisikika kwenye video hiyo akimwambia kuwa pesa hizo ni zawadi kwa siku yake ya kuzaliwa ambayo inakaribia hivi karibuni.

"Kheri ya Siku yako ya kuzaliwa. Nasema tukutunze. TunakupeNda sana. Ata kama uliniacha, mimi pia nimekasirika sana. Happy Birthday,” Zuchu alisikika akimwambia mama huyo bosi wake huku akimkabidhi pesa.

Baada ya kumkabidhi pesa hizo, mtunzi huyo wa kibao  ‘Sukari’ alimbusu Mama Dangote na kumkumbatia huku akimtakia heri ya siku ya kuzaliwa.

Wawili hao walionekana kuwa na wakati mzuri pamoja na kufurahiya sana huku hayo yote yakifanyika.

Sio mara ya kwanza kwa Mama Dangote kuzawadiwa na mrembo huyo anayedaiwa kuwa ni binti mkwewe. Zuchu katika siku za nyuma amewahi kumnunulia mama huyo wa bosi wake zawadi za maalum kama njia ya kumsherehekea.

Mwezi Machi, alionyesha furaha yake baada ya binti huyo wa gwiji wa taarab Khadija Kopa kumzawadia dera zuri.

Mzazi huyo wa bosi wa WCB alionyesha video yake akiwa amevalia dera ambalo alifichua kuwa lilikuwa ni zawadi kutoka kwa Zuchu.

Kwenye video hiyo, Mama Dangote alimshukuru msanii huyo wa mwanaye kwa zawadi maalum na kuonyesha wazi kuwa ameipenda.

"Asante @officialuchu kwa dera zuri!" aliandika.

Dera hilo lilikuwa zawadi maalum ya Zuchu kwa mamake Diamond wakati yeye na waislamu wengine wakiadhimisha mwezi mtukufu wa Ranadhan.

Mapema mwaka huu, Diamond Platnumz alitangaza kuvunjika kwa mahusiano yake na msanii huyo wa lebo yake ya WCB.

Katika taarifa yake, Diamond aliweka wazi kwamba yeye na Zuchu sio wapenzi tena. Alibainisha kuwa yeye na malkia huyo wamebaki kuwa kaka na dada licha ya awali kuonyesha mahaba makubwa  kati yao.

"Kwa pamoja na Zuhura tunaomba tuwataarifu ya kwamba, kwa sasa sisi ni dada na kaka na si wapenzi kama ilivyokuwa ikidhaniwa ama wengine kujua.. Mnaruhusiwa wachumba na wake ama waume kama tutawaridhia," alisema.

Diamond aliongeza, "Lakini muwe na vibarua vinavyoeleweka  sio mje kutuchuna, maana atuhongi hovyo."