Mkewe Guardian Angel, Esther Musila afunguka mkojo wa mamake ulivyomsaidia kupata kazi benki

Musila amesimulia jinsi alivyowasilisha mkojo wa mamake kwa vipimo vya ujauzito kabla ya kupata kazi ya benki.

Muhtasari

•Bi Esther Musila alifichua kuwa lilikuwa ni hitaji la benki kwa wanawake kupimwa ujauzito kabla ya kuajiriwa.

•Musila alipata kazi hiyo baada ya kuwasilisha mkojo wa mama yake na alifanya kazi katika benki kwa takriban miaka sita.

na marehemu mama yake.
Esther Musila na marehemu mama yake.
Image: INSTAGRAM

Mke wa mwimbaji wa nyimbo za injili Guardian Angel, Bi Esther Musila amefunguka kuhusu jinsi alivyowasilisha mkojo wa mama yake kwa vipimo vya ujauzito kabla ya kupata kazi ya uhasibu kati benki moja nchini.

Katika mahojiano ya wazi na KTN, mama huyo wa watoto watatu wakubwa alifichua kuwa lilikuwa ni hitaji la benki alilotaka kufanyia kazi kwa wanawake kupimwa ujauzito kabla ya kuajiriwa.

Wakati ambapo alikuwa akiomba kazi, alikuwa amembeba mtoto wake wa kwanza tumboni, hivyo alijua angefeli mtihani.

“Mama alinipa mkojo wake. Nilijua nina mimba. Nilihitaji kwenda kwenye mahojiano ya kazi. Nilisafiri na mkojo wa mama yangu kutoka Nakuru hadi Nairobi,” Esther Musila alisema.

Malkia huyo mwenye umri wa miaka 53 kwa bahati alipata kazi hiyo baada ya kuwasilisha mkojo wa mama yake na alifanya kazi katika benki kwa takriban miaka sita.

Baada ya miaka sita ya utumishi, alijiuzulu kutoka benki hilo ili kuwatunza watoto wake ambao walikuwa wadogo sana wakati huo. Alikuwa na umri mdogo wa miaka 26 tu wakati alipojiuzulu kutoka benki.

“Niliondoka, nikakaa nyumbani kwa miaka minne, kisha nikahisi nahitaji kuwa na pesa zangu. Hili jambo la kuomba omba pesa halinifanyii kazi,” alisema.

Ni baada ya mtoto wake mdogo kujiunga na shule ambapo alituma maombi ya kazi katika ofisi za Umoja wa Mataifa zilizo Gigiri, Nairobi na kuipata.

“Niliona kazi ikifunguliwa UN, ilikuwa ya miezi mitatu, ilikuwa ni nafasi ya uzazi na nikaomba. Nilijua nitakuwa huko kwa muda wa miezi mitatu pekee,” alisema.

Kwa bahati nzuri, alipata fursa ya kuendelea kutoa huduma zake katika ofisi za Umoja wa Mataifa hata baada ya kupita kwa miezi mitatu ambayo alikuwa amepewa na amekuwa akifanya kazi huko kwa takriban miaka ishirini na miwili iliyopita.

Mwezi uliopita, mhasibu huyo aliweka wazi kwamba bado ana miaka 12 kabla ya kufikia umri wa kustaafu katika Umoja wa Mataifa lakini akadokeza kuwa hataki kusubiri ila badala yake anapanga kustaafu mapema.

”Kwa wale mnaouliza baada ya kuona mahojiano yangu, umri wa kustaafu katika UN ni miaka 65! Bado nina miaka 12 zaidi ya kufanya kazi nikitaka, lakini nina chaguo la kuondoka mapema..,” alisema Esther Musila.