"Nahisi kama naacha tumbo nyuma" Akothee azungumzia wakati wa hisia anapotengana na wanawe

Wanawe Akothee, Prince Ojwang na Prince Oyoo wanaishi na baba mtoto wake wa mwisho mzungu nchini Ufaransa.

Muhtasari

•Akothee alifichua kwamba aliondoka jijini Paris, Ufaransa bila kuonana na wanawe wawili wadogo, Prince Ojwang na Prince Oyoo.

•Wakati pekee ambao siwezi kutabasamu ni wakati wa kuondoka Paris, ninahisi kama ninaacha tumbo langu nyuma, " Akothee alisema.

Akothee na wanawe Prince Oyoo na Prince Ojwang
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee sasa amerejea nchini baada ya kuwa Ulaya kwa wiki kadhaa.

Katika taarifa yake siku ya Ijumaa, mama huyo wa watoto watano ambaye katika siku kadhaa zilizopita amekuwa akifurahia muda na mumewe Denis Shweizer alifichua kwamba alilazimika kurudi nchini Kenya ili kuhudhuria hafla ya binti yake mmoja baadaye mwezi huu.

Hata hivyo alidokeza kuwa hatakuwa nchini kwa muda mrefu kwani anapanga kusafiri kurejea Ulaya baada ya hafla hiyo.

"Ilinibidi nirudi kwa hafla ya binti itakayofanyika tarehe 29 kisha nipande ndege tena hadi kwa mume wangu na watoto," Akothee alisema.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alifichua kwamba aliondoka jijini Paris, Ufaransa bila kuonana na wanawe wawili wadogo, Prince Ojwang na Prince Oyoo.

Alizungumza kuhusu jinsi inavyokuwa kipindi cha hisia kila mara anapowatembelea wavulana hao na hatimaye inafika wakati wa kuondoka.

"Niliondoka Paris bila kuwaona wavulana wangu, wako kwenye safari ya shule kwa wiki mbili kupiga kambi. Uzazi mwenza huu sio wa kila mtu. Wakati pekee ambao siwezi kutabasamu ni wakati wa kuondoka Paris, ninahisi kama ninaacha tumbo langu nyuma, "alisema.

Sambamba na hayo, mama huyo wa watoto watano aliwapongeza wanaume wote kama mumewe Shweizer ambao walikubali kuoa wanawake wanaoshirikiana na wanaume wengine katika malezi na kudokeza kuwa si rahisi.

Katika chapisho lingine, Akothee alichapisha video yenye hisia kali akimuaga mumewe na katika maelezo, alishangaa ni kwa muda gani atalazimika kusafiri kati ya Kenya na Ulaya huku akijaribu kusawazisha maisha yake.

‘Nachukia kwaheri. Nitakumiss mpenzi,” alisema.

Jumamosi asubuhi alithibitisha kuwa tayari yuko nchini Kenya na mara moja akajitosa kwenye shughuli na mambo ambayo alikosa sana wakati akiwa Ulaya kama vile kucheza densi huku muziki ukicheza kwa sauti ya juu.

"Sijakuwa nyumbani tangu miezi," alisema.