"Najua viingereza sio vitu vyenu!" Zari awashambulia mashemeji wa zamani kwa kudai anaishi maisha feki

Mwanasosholaiti Zari Hassan ameendeleza vita vyake vikali na mashemeji wake wa zamani, Watanzania.

Muhtasari

•Zari alionyesha maisha yake ya kifahari na kutumia fursa hiyo kujibu madai ya baadhi ya Watanzania kwamba amekuwa akiishi maisha ya uwongo.

•“Sidhani kama mnajua ‘fake’ nini. Najua viingereza sio vitu vyenu. Fake mnajua ni nini? Hii inaitwa soft life sio fake life," Zari alisema.

Zari Hassan
Image: Zari Hassan Instagram

Mwanasosholaiti mashuhuri wa Uganda, Zari Hassan ameendeleza vita vyake vikali na mashemeji wake wa zamani, Watanzania.

Siku ya Jumanne, mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 42 ambaye anaishi Afrika Kusini alichapisha video iliyoonyesha maisha yake ya kifahari na kutumia fursa hiyo kujibu madai ya baadhi ya Watanzania kwamba amekuwa akiishi maisha ya uwongo.

Zari amekuwa akikabiliwa na madai kuwa anaonyesha maisha ya uwongo mitandaoni ilhali mambo si sawa katika maisha halisi.

"Kurudi kwenye soft life. Sijui nani asiyependa maisha haya fake. Kujipa moyo tu,” Zari alisema kwenye video iliyomuonyesha akiwa pamoja na watoto wake wawili na Diamond, Tiffah Dangote na Prince Nillan na dereva wao wakiwa kwenye moja ya magari yake ya kifahari.

Katika video hiyo aliyoichapisha kwenye mtandao wa Instagram, aliendelea kusisitiza “Hakuna asiyependa hii fake life mwenzangu. Mi sijui asiyependa maisha haya fake. Nani asiyependa maisha haya. Mnajipa moyo wadada wa mjini, mnajipa moyo.”

Mama huyo wa watoto watano alidai kuwa wanaomkosoa hawajui kutofautisha maisha ya ‘fake’ na ‘soft’ ndiyo maana wamekuwa wakimshtumu kuwa haishi maisha halisi.

“Sidhani kama mnajua ‘fake’ nini. Najua viingereza sio vitu vyenu. Fake mnajua ni nini? Hii inaitwa soft life sio fake life. Inaitwa soft life wakati uko na pesa. Mnafaa mjue tofauti,” Zari Hassan alisema.

Hatua hii ya hivi punde inaonyesha kuendelea kwa vita kali kati ya Zari  Hassan na Watanzania.

Takriban wiki tatu zilizopita, mpenzi huyo wa zamani wa staa wa bongo Diamond Platnumz na Watanzania walikuwa wakibadilishana maneno mitandaoni, mada kuu ikiwa ni mume wake wa sasa, Shakib Cham Lutaaya.

Watanzania kadhaa watumizi wa mtandao wa Instagram walimshambulia Zari kuhusu umri wa mumewe na mwonekano wake hadharani. Baadhi waliibua wasiwasi kuhusu pengo kubwa la umri kati ya wanandoa hao huku wengine wakidai kwamba Shakib alionekana kutokuwa na raha wakati akiwa na mama huyo wa watoto watano.

"Lakini nyie Waafrika, kijana awe mdogo, hana raha au vipi, tatizo lako ni nini? Je,  (Zari) ni wewe?  (Shakib) ni wewe? Waruhusu watu waishi maisha yao kwa njia zao, kwa matakwa yao. Pelekeni hisia huuuko!!" Shabiki mmoja alibainisha kwenye sehemu ya maoni ya chapisho la hivi majuzi la Zari kwenye Instagram.

Huku akikubaliana na maoni ya shabiki huyo, mwanasosholaiti huyo alibainisha, "Sio Waafrika, ni Watanzania!"

Zari alishangaa ni kwa nini Watanzania wanapenda kulalamika linapokuja suala la mahusiano yake ilhali hawapati shida ya kukosoa wakati mtu mwingine anafanya jambo sawa.

"Ni Tanzania pekee ambapo ikikuja kwangu, wanaume wa miaka 32 wanachukuliwa kama watoto. Sijawahi kuona watu wabaya kama wao," Zari alisema.

Mwanasosholaiti huyo ambaye alionekana kuchoshwa kabisa na raia wa nchi hiyo jirani aliwataka wajali mambo yao wenyewe.

"Watanzania bana.. sijui mdogo, sasa ni mzee. Hacheki, oh leo kafosiwa.. Mmepotoshwa. Yenu ni kuangalia ya watu. Aai, kwa mara moja mjali maisha yenu wenyewe," alimjibu shabiki aliyedai mumewe anaonekana mzee.

Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz aliwataka mashemeji hao wake wa zamani kusonga mbele na maisha yao sasa akibainisha kwamba tayari miaka mitano imepita tangu aondoke Tanzania.