"Ni rafiki tu" Zuchu amkana waziwazi Diamond kuwa mpenziwe huku akieleza kwa nini alimbusu

Katika jibu lake, Zuchu alidai kwamba aliwezwa na hisia na kujipata amembusu bosi huyo wake.

Muhtasari

•Zuchu alibainisha kuwa Diamond amekuwa akimnunulia mapambo ya gharama ya mamilioni ya pesa kama rafiki na msanii wake tu.

•Mwimbaji huyo wa kibao ‘Sukari’ alibainisha kuwa matukio kama hayo ya kimapenzi hutokea tu katika nyakati maalum.

Diamond na Zuchu warekodiwa wakipatiana mabusu.
Diamond na Zuchu warekodiwa wakipatiana mabusu.
Image: Screengrab

Malkia wa Bongofleva Zuhura Othman almaarufu Zuchu amesisitiza kuwa uhusiano kati yake na bosi wake Diamond Platnumz ni urafiki wa kirafiki tu.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na Wasafi Media, msanii huyo kutoka Zanzibar alibainisha kuwa Diamond amekuwa akimnunulia mapambo ya gharama ya mamilioni ya pesa kama rafiki na msanii wake tu.

Zuchu pia alilazimika kueleza kuhusu video iliyovuma ambayo ilionyesha matukio ya kimapenzi huku yeye na bosi huyo wa WCB wakikumbatiana na kubusiana uwanja wa ndege. Katika jibu lake, alidai kwamba aliwezwa na hisia na kujipata amembusu  bosi huyo wake.

“Ni rafiki tu, nilikuwa nasindikiza boss wangu airport nikamkumbatia maybe I got a little emotional ikabidi nimpe na kabusu,”Zuchu alisema.

Mwimbaji huyo wa kibao ‘Sukari’ alibainisha kuwa matukio kama hayo ya kimapenzi hutokea tu katika nyakati maalum.

Mapema wiki hii, video ya mastaa hao wawili wa bongo wakibusiana na kukumbatiana kimahaba kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere nchini Tanzania wakati Diamond akijiandaa kuelekea nchini Canada kwa ziara ya kimuziki ilivuma kwenye mitandao ya kijamii na kuzua hisia mseto baina  ya wanamitandao. Wengi walionekana kushawishika kuwa wawili hao ni wapenzi licha ya mara nyingi kudai kuwa marafiki tu.

Katika mahojiano hayo, Zuchu aliiri kuwa alijawa na ghadhabu na kusababisha fujo baada ya kumuona bosi yake Diamond akimbusu Fantana kwenye filamu ya Young, Famous na African .

Alikiri kuwa ni kweli alivunja vitu ndani ya nyumba ya Diamond baada ya kuona sehemu ambapo bosi huyo wa WCB alimbusu mshirika huyo wake kwenye YFA2. Alifichua kuwa wakati huo alikuwa akifanya usafi ndani ya nyumba ya Diamond alipoona video hiyo kwenye Snapchat.

“Kweli nilivunja vitu. Ilitokea. Nilikuwa nimekasirikasana. Niliona rafiki yangu amevuka mipaka. Hayo sio mambo unafanya kwenye runinga rafiki,” Zuchu alisimulia.

Aliendelea, “Kwa kweli nilikuwa nyumbani kwake. Nilikuwa bize nikiosha nyumba na nilikuwa napanga glasi nikawa nimeshika simu nikaingia snapchat. Niliona ile scene, nikawa najiuliza kama ni video ya kweli nikasema hapana nimekataa.”

Zuchu alifichua kuwa aliwahi kukutana na Fantana hapo awali wakati wa kurekodi kwa filamu hiyo nchini Afrika Kusini.

Hata hivyo alisema kuwa tukio la Diamond kumbusu mwimbaji huyo wa Ghana lilimpata kwa mshtuko na kumfanya akasirike.

"Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuona scene hiyo kama kila mtu mwingine. Moyo wangu ulivunjika. Sikujua la kufanya na nilikuwa nikimpigia simu, nadhani alikuwa ikulu siku hiyo ikawa hapokei simu, nadhani kwa sababu alikuwa bize,” alisema.

Zuchu alieleza kuwa ni baada ya bosi wake kukosa kuchukua simu yake ndipo alifanya fujo kutokana na hasira kwani hakuweza kuzungumza na mtu yeyote. Alikiri alipiga kelele tu huku akivunja vitu ndani ya nyumba ya bosi huyo wake  kabla ya kuondoka na vitu vyake.

“Baadaye alikuwa akinipigia simu na sikuwa nikipokea simu zake. Sikutaka tu kuzungumza naye. nilikuwa nimemalizana naye,” alisema..

Malkia huyo wa bongofleva alisema kuwa Diamond aliendelea kujaribu kumpigia simu hadi akapokea mida ya saa tisa usiku na bosi huyo wa WCB akamweleza kwanini hakuwa akipokea simu yake.

“Kuna changamoto nyingine, nadhani sijui ananiweza sana. Nimekuwa mrahisi sana kwake. Sikuwa hivi, niamini, huwa sipatiani nafasi za pili. Sijui kwa nini na yeye,” alisema.

Alifichua kuwa alimtumia Diamond ,ambaye anasisistiza ni rafiki wake tu, video hiyo ya busu ambaye na kumfahamisha kuwa hiyo ndiyo sababu ya hasira yake.

“Naweza kuwa nimefungwa macho na mapenzi lakini sidhani niko chini sana kuwa kipofu. Nahisi kama maelezo aliyonipa ilinipa muda kuifuta lakini ilifika hatua nikaamua kumsamehe… Nadhani ni vizuri kwenye mapenzi mtu akawa huru kufanya chochote anachotaka.Kwa hivyo yeye kama kaamua kuwa hivyo, wacha awe hivyo. Afanye kwa uwezo wake, siku nitajiona nimechoka nitamuacha,” Zuchu alisema.