Niko na kundi la WhatsApp na baby daddies wangu- Akothee afichua huku akimsfia ex wake Nelly Oaks

Akothee aliwashangaza wengi baada ya kufichua kuwa ana kikundi cha WhatsApp na wazazi wenzake.

Muhtasari

•Akothee ni mama wa watoto watano, wasichana watatu na wavulana wawili, ambao wote alipata na wapenzi wake wa zamani watatu.

•Akothee alikuwa akitambua majukumu makubwa ya Nelly Oaks na kueleza kwa nini si rahisi kuwa meneja wake.

Akothee na Nelly Oaks
Image: INSTAGRAM

Wikendi, mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee aliwashangaza wengi baada ya kufichua kuwa ana kikundi cha WhatsApp na wazazi wenzake.

Mama huyo wa watoto watano aliowapata na wanaume watatu tofauti alifichua hayo wakati akimsifia meneja wake na ambaye ni mpenzi wake wa zamani, Nelly Oaks mbele ya wageni wachache waalikwa waliokuwa wamehudhuria uzinduzi wa biashara ya bintiye Vesha Akello siku ya Jumamosi jioni.

Alikuwa akitambua majukumu makubwa ya Nelly Oaks na kueleza kwa nini si rahisi kuwa meneja wake.

"Niruhusu nimtambulishe mwanamume aliye nyuma ya chapa yangu, rafiki yangu bora. Jamaa huyu ana moyo mkubwa, kumshughulikia Akothee si kitu karibu na kumshughulikia Raila au Uhuru au Ruto,” Akothee alisema.

Aliongeza, "Kushughulikia mwanamke aliye na kikundi cha WhatsApp na baba wa watoto, mbwembwe, muziki.. tafadhali mpigieni makofi Nelly Oaks ."

Hata hivyo, hakufichua maelezo mengi kuhusu kikundi hicho cha WhatsApp na ikiwa kinajumuisha wazazi wenzake wote ama jinsi kinavyofanya kazi.

Mwimbaji huyo aliendelea kueleza kwa nini Nelly Oaks atakuwa karibu naye kila wakati licha ya kutengana kwao kimahusiano.

Alimtaja kama sehemu ya familia yake na akamshukuru kwa kusimamia chapa ya Akothee na kuwatunza watoto wake.

“Tunatoka mbali. Babu yake aliacha urithi katika jamii yangu. Unapomwona Nelly karibu nami, sijali unachotaka kufikiria.. Nelly asante kwa kuwa kila wakati kwa chapa ya Akothee na kwa kuwa kila wakati kwa watoto wangu. Anawatunza watoto wangu. Wanatoka pamoja, wanacheza densi. Wanangu wanampigia simu kila siku. Unapotuona, sisi ni familia," alisema.

Akothee ni mama wa watoto watano, wasichana watatu na wavulana wawili, ambao wote alipata na wapenzi wake wa zamani watatu.

Watoto wake watatu wa kwanza ni wasichana na aliwapata na mume wake wa kwanza, Jared Okello ambaye alitengana naye zaidi ya mwongo mmoja uliopita.

Wavulana wake wawili, Prince Ojwang na Prince Oyoo, wanaishi Ufaransa na baba wa mtoto wake wa mwisho Prince Oyoo.