Nilikuwa tayari kushare Samidoh nikawachiwa roho safi- Karen Nyamu aweka mambo wazi

Nyamu alidokeza kwamba Bi Edday ndiye aliyemuachia mwimbaji huyo wa Mugithi kwa hiari.

Muhtasari

•Karen Nyamu amedokeza kwamba alikuwa tayari sana kuwa mke mwenza wa mke wa Samidoh, Bi Edday Nderitu.

•Kwa kufafanua seneta huyo wa UDA alisema, “Nikawachiwa roho safi.”

Image: INSTAGRAM// KAREN NYAMU

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amedokeza kwamba alikuwa tayari sana kuwa mke mwenza wa mke wa mwimbaji Samuel Muchoki almaarufu Samidoh, Bi Edday Nderitu.

Huku akiwajibu mashabiki kwenye mtandao wa Facebook, mama huyo wa watoto watatu alisema kwamba Edday ndiye aliyemuachia mwimbaji huyo wa Mugithi kwa hiari.

Katika ujumbe wa kimafumbo Karen alisema, "Nilikuwa tayari kushare lakini ..."

Shabiki mmoja alisema, "Ukachukua yote"

Lakini huku akifafanua  kwa utani, seneta huyo wa UDA alisema, “Nikawachiwa roho safi.”

Karen Nyamu alitoa maoni hayo katika chapisho lake kuhusu sherehe ya kuhitimu ya kaka mdogo wa Samidoh ambayo alikuwa amehudhuria siku ya Jumanne jioni.

"Jana usiku tulikusanyika ili kusherehekea kijana mmoja wa kufurahisha na ya kupendeza. Hongera kwa kuhitimu kwako Amo. Wewe ni nyota anayekuja,” Karen Nyamu aliandika siku ya Jumatano.

Aliambatanisha taarifa hiyo na picha zake akiwa na Samidoh, kaka yake mdogo na baadhi ya watu wengine waliohudhuria sherehe hiyo.

Mkewe Samidoh, Bi Edday Nderitu amekuwa akizozana na Karen Nyamu kwa muda mrefu tangu seneta huyo wa kuteuliwa kuingia katika ndoa yao miaka kadhaa iliyopita. Seneta Nyamu amekuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwimbaji huyo wa Mugithi kwa muda sasa na wawili hao tayari wana watoto wawili pamoja.

Katika wiki kadhaa za hivi majuzi, Samidoh ameonekana kutumia muda mwingi na seneta Nyamu huku mkewe Edday Nderitu akiaminika kuwa Marekani. Bado haijabainika wazi madhumuni ya ziara ya Edday nchini Marekani au ikiwa ndoa yake na Samidoh ya zaidi ya mwongo mmoja bado iko hai.

Mwezi Februari, Bi Edday alimwandikia Samidoh ujumbe mrefu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akimuonya kwamba hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi. Hii ilikuwa baada ya msanii huyo kuonekana na mzazi mwenzake, Karen Nyamu licha ya awali kudaiwa uhusiano wao umefika mwisho.

Edday alimtaja Bi Nyamu kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake. Alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi. Hata hivyo, alisema licha ya yote amebaki mwaminifu na ameendelea kuunga mkono kazi ya msanii huyo wa nyimbo za Kikuyu. 

"Nimebaki mwaminifu kwako bila kujali kudharauliwa, kudhalilishwa na kutukanwa kwenye mitandao ya kijamii, umenifanya nionekane mjinga na kuchukulia ukimya wangu kuwa wa kawaida, nimekusaidia kuinua kipaji chako na kukuunga mkono kwa yote, lakini kitu kimoja nimekwambia na nasema hapa tena sitalea watoto wangu katika familia ya wake wengi," alisema kwa uchungu.

Alibainisha kuwa ndoa yake ilikuwa nzuri siku za awali kabla ya mtu wa tatu kuingia ndani yake takriban miaka mitatu iliyopita.