Ningeendelea kukaa kwenye ndoa na Omosh, maisha yangu yangekuwa mafupi- Akothee

Akothee alifichua kuwa hangeweza kuendelea na ndoa hiyo baada ya mambo aliyogundua wakati wa fungate.

Muhtasari

•Akothee alifichua alianza kuondoka kwenye ndoa hiyo baada ya fungate kwani angehatarisha maisha yake kwa kuendelea kukaa.

•Alidokeza kuwa hali ya ustaa ilimletea upweke maishani na alipata faraja kubwa kwa mzungu huyo kutoka Uswizi walipokutana.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mtumbuizaji wa Kenya, Esther Akoth almaarufu Akothee ameendelea kufunguka mengi zaidi kuhusu ndoa yake ya muda mfupi na Denis ‘Omosh’ Schweizer.

Katika taarifa yake Alhamisi asubuhi, mama huyo wa watoto watano alifichua kuwa hangeweza kuendelea na ndoa hiyo baada ya mambo aliyogundua wakati wa fungate.

Akothee alifichua kuwa alianza kuondoka kwenye ndoa hiyo baada ya fungate yao iliyofanyika Santorini, Ugiriki kwani angehatarisha maisha yake kwa kuendelea kukaa.

"Mkweli na mjinga, lakini hiyo hainifafanui mimi kama mtu binafsi. Ninashinda katika masuala mengi, nilipoteza katika hii ni sawa. Nilianza mpango wangu wa kuondoka baada ya fungate, sijui jinsi ya kulazimisha mambo ya mapenzi, hasa baada ya kujua ninachojua sasa,” Akothee alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aliongeza, “Kama ningeendelea na simulizi ya kukaa kwenye ndoa hii baada ya yote ninayoyajua sasa, maisha yangu yangekuwa mafupi kuliko aya fupi zaidi katika biblia 🙏 , ilinibidi nijilinde na akili yangu iliyobaki ni historia, 🙏 Iko vizuri 🙏."

Muimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 aliweka wazi kuwa sasa tayari amepona maumivu yaliyofuatia kuvunjika kwa ndoa yake mwezi Juni mwaka huu.

Katika taarifa yake, alifichua kuwa Omosh alikuja maishani mwake katika muda ambao alikuwa tayari kutulia na alimpa mengi aliyohitaji.

Alidokeza kwamba hali ya ustaa ilimletea upweke maishani na alipata faraja kubwa kwa mzungu huyo kutoka Uswizi walipokutana.

“Nilipata faraja kwa Denis. Alionekana kama mechi kamili kwa miezi hiyo michache. Naweza kusema nilipuuza tahadhari zote;

Nilijiaminisha kuwa huyu ndiye aliyenifaa. Nilikuwa, na bado sina hatia. Nimejisamehe kwa kutokuwa na akili,” alisema.

Akothee alikuwa akizungumza kuhusu mkutano wake wa hivi majuzi na wakili maarufu wa Kenya, Miguna Miguna na kumtambua kwa sapoti yake wakati alipofichua maelezo kuhusu ndoa yake iliyovunjika na Bw Schweizer.

Akizungumza wakati wa kipindi cha moja kwa moja mnamo Jumanne usiku, mwanamuziki huyo alidokeza kuwa aligura ndoa yake walipokuwa wakifurahia fungate  baada ya kujifunza mambo kadhaa ambayo hakujua hapo awali.

Hata hivyo alidokeza kwamba hakumwambia mzungu huyo kutoka Uswizi kuhusu uamuzi wake mara moja na hata walipokuwa wakiagana, alimdanganya kwamba hangemuacha.

"Nilitoka nje ya uhusiano mnamo Juni. Kawaida mimi hutoka nje ya uhusiano wangu wakati bado niko kwenye uhusiano. Tulipokuwa kwenye fungate, niligundua mambo fulani ambayo sikuweza kustahimili. Kisha akaniuliza, “Utaniacha?” Nikasema, "hapana mpenzi nakupenda". Nilipokuwa nikitoka Uswizi mnamo Julai, kwenye uwanja wa ndege aliniuliza," utaniacha?, Nikasema "hapana mpenzi, nakupenda". Lakini kwa hakika, nilikuwa tayari nimeondoka,” Akothee alisimulia