"Nini ilikuwa inanisumbua!" Akothee ajuta kutoroka shule, kuolewa akiwa na umri wa miaka 14

“Kwani kulikuwa na nini kwenye ndoa nikiwa na miaka 14? Ni nini ilikuwa inanisumbua?” Akothee alishangaa.

Muhtasari

•Akothee amefunguka jinsi alivyogura shule hiyo iliyo katika Kaunti ya Migori ili kwenda kuolewa akiwa na umri mdogo sana.

•Mama huyo wa watoto watano alishangaa kwa nini alikuwa na haraka ya kuolewa hadi kufikia hatua ya kutoroka shule.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Siku ya Jumapili, mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee alishiriki picha yake akiwa amesimama kando ya ishara ya Shule ya Upili ya Wasichana ya Nyabisawa.

Katika sehemu ya maelezo, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alifunguka jinsi alivyogura shule hiyo iliyo katika Kaunti ya Migori ili kwenda kuolewa akiwa na umri mdogo sana.

Alifichua kuwa kila anapopita shule hiyo yake ya zamani huwa anakumbwa na majuto ya kwa nini alivunja moyo wazazi wake kwa kutoroka shule ili kuanza familia.

“Hii ndiyo shule niliyoiacha nikiwa na umri wa miaka 14 nikikimbia kuwa mke. Kila ninapopita hapa nikielekea THIM LICH, huwa najisikia vibaya sana kwa nini nililazimika kuwaumiza wazazi wangu kiasi hiki,” Akothee alisema chini ya picha hiyo aliyoichapisha kwenye mtandao wa Instagram.

Mama huyo wa watoto watano alishangaa kwa nini alikuwa na haraka ya kuolewa hadi kufikia hatua ya kutoroka shule.

“Kwani kulikuwa na nini kwenye ndoa nikiwa na miaka 14? Ni nini ilikuwa inanisumbua?” aliandika.

Mapema mwezi huu, Akothee aliitaja ndoa yake ya kwanza na baba wa mabinti zake watatu, Jared Okello kama mazoezi ya ndoa tu.

Alibainisha kwamba alikuwa mdogo sana wakati alipoolewa mzazi huyo mwenzake na alijua kidogo sana kuhusu ndoa.

"Nilikuwa na umri wa miaka 14, nilijua nini? Msichana wa miaka 14 anajua nini kuhusu ndoa?" Akothee alihoji.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 aliendelea kueleza mazingira yaliyompelekea kufanya harusi na Bw Jared Okello. 

Alifichua kwamba mume huyo wake wa zamani alikuwa asafiri kuenda nchini Marekani na njia pekee ambayo yeye na watoto wao wangemfuata huko ilikuwa kwanza kufunga ndoa rasmi naye.

"Ex wangu alikuwa akienda Bahamas na watu wa SDA. Alitaka kurudi kunichukua pamoja na watoto. Njia pekee ambayo angeniongeza kwenye orodha yake ya kusafiri, ni kwa sisi kufunga ndoa. Harusi yangu iligharimu shilingi 2,500,” alisema.

Mwanamuziki huyo aliweka wazi kuwa bajeti yao ya harusi ya 2,500 ilishughulikia kila kitu kilichofanyika ama kutumia siku hiyo.

Alidokeza kwamba ndoa yake na Bw Jared iligonga ukuta baada ya baba huyo wa binti zake watatu kumpenda mwanamke mwingine.

Baada ya kutengana na Bw Jared, mwimbaji huyo alielekea Mombasa ambako alinuia kujiingiza katika shughuli ya kumpa riziki.

"Siku zote nilitaka kuwa dereva wa teksi. Sikuwa na karatasi za kwenda kugonga mlango wa mtu, nilikuwa na karatasi za kidato cha 4 tu. (Bw Jared) Alikataa na hati zangu pamoja na kitambulisho changu. Nilipoenda Mombasa singeweza kupata kazi yoyote, hata kuwa mhudumu inahitaji kitambulisho,” Akothee alisimulia.

Ni wakati alipokuwa Mombasa ambapo alikutana na baba yake mtoto wake wa nne ambaye alizaa naye mtoto mvulana wake wa kwanza, Prince Ojwang.