"Omba msamaha unaweza kufikiriwa!" Harmonize amshauri Kajala huku vita vyao vikipamba moto

Harmonize amefichua alikuwa akigawa sehemu ya mapato yake kwa Kajala na hata alimpa nambasiri za kadi zake zote za benki.

Muhtasari

•Harmonize amebainisha kuwa anafurahia vita vya mtandaoni kati yake na muigizaji huyo  badala ya kuumia moyo.

•Harmonize amembainishia Kajala kuwa sasa anaingiza pesa nyingi zaidi kuliko alivyokuwa akipata kipindi walichokuwa wakichumbiana.

Harmonize na aliyekuwa mpenzi wake Kajala
Image: HISANI

Bongo kumewaka moto, wapenzi wa zamani Harmonize na Kajala Masanja wamejikita katika vita vya hadharani kwenye mitandao ya kijamii.

Vita hiyo ilianza baada ya bosi huyo wa Konde Music Worldwide kuachia wimbo ‘Dear Ex’ ambapo alilalamika kuhusu jinsi Kajala na bintiye Paula walimtenda vibaya wakati muigizaji huyo alimtema mwishoni mwa mwaka jana.

Jumatano mchana, Kajala alionekana kujibu shutuma za staa huyo wa bongo fleva kwa kuchapisha video yake na bintiye wakicheka, jambo ambalo linaonekana kumkera bosi huyo wa Kondegang.

Katika majibu yake, Konde Boy alibainisha kuwa familia hiyo yake ya zamani inaonekana kuwa ilikuwa ikisubiri kwa hamu wakati huu.

“Unaweza kuona jinsi walivyosubiri wakati huu. Dakika tu washajibu. Tunasisitiza mseme na mema sio kujichekesha and 2B tu!” Harmonize alisema kupitia Instagram.

Mwimbaji huyo alibainisha kuwa anafurahia vita vya mtandaoni kati yake na muigizaji huyo mkongwe badala ya kuumia moyo kama ilivyotarajiwa.

Wakati huohuo, aliendelea kufichua maelezo ya kushangaza kuhusu jinsi alivyokuwa akigawa sehemu ya mapato yake kwa mpenzi huyo wake wa zamani na jinsi hata alivyompa nambasiri za kadi zake zote za benki.

“Simulia basi hapo kwenye TV kwamba nilikuwa nakupatia 10% ya kila ninachoingiza kwenye shows, endorsement, kila kitu. Waambie ulikuwa na pin ya kila kadi zangu za benki.

“Bahati haiji mara mbili. Huwezi kuwa na furaha kiasi hicho ikiwa umevunja gari kutoka kwenye range kurudi kwenye Toyota. Ungenipigia simu nikusaidie hela ya huduma. Mimi ni mtu mzuri unalijua hilo,” alisema.

Mwimbaji huyo wa kibao ‘Single Again’ alimbainishia mpenzi huyo wake wa zamani kuwa sasa anaingiza pesa nyingi zaidi kuliko alivyokuwa akipata katika kipindi walichokuwa wakichumbiana mwaka jana.

Aidha, alimshauri zaidi kutumia njia sahihi za kuomba msamaha akidokeza kwamba kuna uwezekano wa kumsamehe kwa kila makosa aliyofanya.

“Lia, sakata menooo, omba msamaha. Unaweza kufikiriwaaa. Ila njia unayotumia hutobo, changanya na umriii. Wacha tuone,”

Konde Boy alimaliza kwa kuweka wazi kuwa hatazungumza zaidi kuhusu mzozo wake na mpenzi huyo wake wa zamani.