Radio yafutilia mbali mahojiano ya DJ Fatxo baada ya mashabiki kulalamika vikali

Kituo hicho kilibaini kuwa mashabiki wake wengi walipinga vikali mahojiano hayo wakidai kuwa ni ya kukera.

Muhtasari

•Kituo hicho cha redio kilibainisha kuwa uamuzi wa kufutilia mbali mahojiano hayo ulifuatia malalamishi mengi kutoka kwa mashabiki. 

•DJ Fatxo amekabiliana na upinzani mkubwa kutoka kwa umma tangu alipohusishwa na kifo cha Jeff ambaye alifariki nyumbani kwake Februari.

Image: FACEBOOK// DJ FATXO

Kituo kimoja cha redio cha humu nchini kilifutilia mbali mahojiano na mwanamuziki Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo siku ya Ijumaa.

Katika taarifa kutoka kwa timu ya Uhusiano wa Umma, kituo hicho cha redio kilibainisha kuwa uamuzi wa kufutilia mbali mahojiano hayo ambayo yalikuwa yafanyike katika kipindi cha asubuhi ulifuatia malalamishi mengi kutoka kwa mashabiki. 

Kituo hicho kilibaini kuwa mashabiki wake wengi walipinga vikali mahojiano na mwanamuziki huyo wakidai kuwa ni ya kukera.

“Kituo kilighairi mahojiano na Lawrence Wagura Njuguna, almaarufu DJ Fatxo ambayo yaliratibiwa leo (Ijumaa, Agosti 18) saa moja asubuhi hadi saa mbili.  Hii ni kutokana na malalamishi ya mtandaoni kutoka kwa mashabiki wetu, ambao walihisi kuwa ilikuwa mbaya. Kama shirika, tunathamini wateja wetu na wasikilizaji wetu, mnakuja mbele,” taarifa ya kituo hicho  ilisomeka.

Katika miezi michache iliyopita DJ Fatxo, ambaye ni mwimbaji wa nyimbo za Kikuyu amekuwa akifanya jitihada za kurejea hadharani na kuendelea na kazi yake ya muziki baada ya kuondolewa madai ya mauaji ya Jeff Mwathi. Fatxo amekabiliana na upinzani mkubwa kutoka kwa umma tangu alipohusishwa na kifo cha kijana huyo wa miaka 23 ambaye alifariki nyumbani kwake mnamo Februari.

Mwezi Mei, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma aliwaondolea DJ Fatxo na wenzake mashtaka ya mauaji ya Jeff Mwathi na kueleza ni kwa nini hakuna hata mmoja aliyekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha kijana huyo wa miaka 23.

Katika barua kwa Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai iliyotiwa saini na mkurugenzi msaidizi wa mashtaka ya umma Gikui Gichuhi, DPP alitaja ushahidi uliowaondolea washukiwa hao mashtaka.

DPP alisema Jeff, ambaye jina lake halisi ni Geoffrey Mwathi Ngugi, alimtembelea DJ Fatxo mnamo Februari 21 kwa ajili ya kazi ya usanifu wa mapambo ya ndani katika biashara yake karibu na Eastern Bypass.

Alisema wawili hao pamoja na marafiki wa Jeff walijivinjari kwa chakula na vinywaji katika baa mbalimbali kabla ya kurejea kwa ajili ya mapumziko katika nyumba ya Fatxo saa tisa usiku wa kuamkia Februari 22. Makao hayo yalikuwa kwenye ghorofa ya 10 ya ghorofa ya Redwood ndani ya mtaa wa Roysambu,  Nairobi.

"Iliripotiwa kuwa marehemu alitoweka kwenye chumba cha kulala cha wageni na mwili wake kupatikana kwenye ghorofa ya chini ya jengo hilo," Haji alisema.

DPP alisema uchunguzi uliofuata, mawasilisho ya mashahidi na matokeo ya uchunguzi kabla na baada ya kuzikwa, yalithibitisha kuwa Jeff Mwathi alikufa katika eneo la tukio ambapo mwili wake ulipatikana.