"Siwezi kumuacha na hiyo pesa yake!" Karen Nyamu afunguka kuhusu kuchezwa, kuachwa na Samidoh

Seneta Nyamu amedokeza kuwa wanaosubiri uhusiano wake na Samidoh kuyumba watalazimika kusubiri kwa muda mrefu.

Muhtasari

•Nyamu aliwataka wanawake kuzingatia afya yao ya akili akibainisha kuwa watoto na waume wanaweza kuwaacha siku moja

•Seneta Nyamu alijibu “Hata mimi siwezi kumuacha na hiyo pesa yake, tafuteni pesa mama.”

Samidoh na Karen Nyamu
Image: HISANI

Siku ya Ijumaa, seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu alizamia kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii kuwashauri wanawake dhidi ya kujiweka katika shinikizo kubwa ili kufurahisha wengine.

Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Instagram, mwanasheria huyo aliwashauri wanawake kujitendea vyema na kufanya kile kinachowafurahisha.

Nyamu aliwataka kuzingatia afya yao ya akili akibainisha kuwa watoto na waume wanaweza kuwaacha siku moja.

"Wanawake: Sio lazima ufanye kila kitu, sio lazima uwe mama bora, mama wa nyumbani bora, mtaalamu wa hali ya juu, mwanamke mkuu. Kwa sababu wakati mwili wako unadai wewe, kutakuwa na wachache ambao watakumbuka ulijaribu kuwa yote katika moja!

Kwa hivyo toka nyumbani, safiri, tembea, fanya mazoezi, nenda kwenye bustani, nenda kwenye ukumbi wa mazoezi, kula kile kinachokukasirisha, jirekebishe, lala baadaye, vaa nguo unazopenda, uwe mwenyewe, jijali, jipende. , sema hapana wakati mwingine na fanya kwa ajili YAKO PEKEE!!" 

Watoto hukua na kuondoka, waume hawabaki kila mara, kazi inaweza kuchukua nafasi yako kwa urahisi, nyumba itachafuka tena, lakini afya yako ya kihisia pia ni muhimu na unaweza usipate nafasi ya pili,” Karen Nyamu aliandika.

Kama kawaida, watumiaji wa mitandao ya kijamii walikuwa na la kusema kulingana na jinsi walivyoelewa ujumbe huo.

Baadhi ya watumiaji wa Instagram waliona kauli ya Karen Nyamu kuwa kidokezo kwamba mambo si mazuri kati yake na mpenzi wake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

“Umeachwa,” Ladonnah_Chepkemoi alimuuliza.

Katika majibu yake, seneta huyo wa UDA alidokeza kuwa wanaosubiri uhusiano wake kuyumba watalazimika kusubiri kwa muda mrefu.

“Utangoja sana. Hii nayo inataka uvumilivu,” Karen Nyamu alijibu.

Shabiki mwingine alibainisha kuwa itakuwa vigumu kwa mwimbaji Samidoh kumwacha Karen Nyamu kwa sababu ya pesa zake.

Mama huyo wa watoto watatu hata hivyo alijibu kwa utani, “Hata mimi siwezi kumuacha na hiyo pesa yake, tafuteni pesa mama.”

Kwenye Facebook, mfuasi mmoja alijaribu kumshauri ajitunze pia akidai kuwa alikubali kuchezewa na mwanamume (Samidoh)  kama mtoto.

“Jiheshimu wewe ni mwanamke mchapakazi. Jina lako linavuma sana hapa USA, Jipende kiasi msichana,” Martha Mburu alimwambia.

Karen Nyamu alijibu, “Mwanaume wangu hajanichezea. Hata hivyo, uko huru kutunga hadithi na kuziamini. Jina linalovuma sio la kila mtu. Vibaya au "vizuri" tunapenda kuvuma."

Hivi majuzi, seneta huyo amekuwa akivuma baada ya kuhusika katika drama ya mtandaoni na promota kutoka nchini Marekani Sue Gachambi.