Stevo azua wasiwasi kwa ujumbe wa hisia huku kukiwa na tetesi za ndoa yake kuvunjika

Kumekuwa na tetesi kuwa ndoa ya rapa huyo iko kwenye mtafaruku baada ya kudaiwa kuumizwa moyo na mkewe.

Muhtasari

•Stevo Simple Boy alishiriki picha ya mkusanyo wa emoji zinazoashiria masikitiko na huzuni ili kueleza hali yake ya sasa.

•Kumekuwa na uvumi kuwa yeye na mkewe Grace Atieno wamekuwa wakikumbwa na matatizo katika ndoa yao baada ya rapa huyo kugundua kuwa ana ujauzito wa mwanaume mwingine.

Mwanamuziki Stivo Simple Boy
Image: HISANI

Msanii mashuhuri kutoka Kibera Stephen Otieno Adera almaarufu Stevo Simple Boy amechapisha ujumbe wa kimafumbo ambao umezua wasiwasi miongoni mwa mashabiki wake.

Katika chapisho lake siku ya Jumatatu, rapa huyo mwenye umri wa miaka 33 alishiriki picha ya mkusanyo wa emoji zinazoashiria masikitiko na huzuni ili kueleza hali yake ya sasa.

Chini ya picha hiyo, aliandika “Vichuna!!!!!!.. Eeeeish” kumaanisha kuwa hali yake ya huzuni ilikuwa na uhusiano na mwanamke au mpenzi wake. Hata hivyo hakushiriki maelezo mengi kuhusu kile ambacho kilikuwa kinamsumbua.

Chapisho la Stevo linakuja huku kukiwa na tetesi kuwa ndoa yake iko kwenye mtafaruku baada ya kudaiwa kuumizwa moyo na mkewe. Kumekuwa na uvumi mwingi ambao haujathibitishwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa yeye na mkewe Grace Atieno wamekuwa wakikumbwa na matatizo katika ndoa yao baada ya rapa huyo kugundua kuwa ana ujauzito wa mwanaume mwingine.

Tazama baadhi ya majibu kwa chapisho la Stevo;

Gtg_ldpc Wamekukulia bana

Jacuzzi_ Pole mzee kila kitu kitakuwa sawa

Taqueen_jk: Dame ashakuliwa

_dayo_dess: Wachana na wasichana Stivo

Duchess_of_kabeteshire: Bet hii ni kiki so wacha ufala

Simple Boy alimtambulisha Grace Atieno kama mke wake halisi hadharani wakati wa hafla ya mazishi ya babake mnamo Februari 11 mwaka huu.

"Bwana asifiwe. Kwa majina mimi ni Stephen Otieno. Mimi ndiye kitinda mimba wa Anthony Adera, na huyu ndiye mke wangu," alisema mwimbaji huyo kabla ya kumpa kipaza sauti mke wake mrembo aliyesimama kando yake.

Baada ya kupokea kipaza sauti, Bi Atieno alimwomboleza baba mkwewe huku akionyesha wazi wazi ukaribu uliokuwepo kati yake na marehemu.

"Bwana asifiwe. Kwa majina ni Grace Atieno. Nimeoleka kwa Bwana Stephen Otieno. Naskia vibaya kumpoteza mtu mwenye alikuwa akinitoa kila wakati..." Grace alisema kabla ya kuzidiwa na hisia na kuangua kilio.

Kwenye mahojiano, Stivo aliweka wazi kwamba kwa sasa anaishi na mwenzi huyo wake wa maisha jijini Nairobi. Aliweka wazi kwamba yeye na Grace wanapendana sana na wanapanga kuendeleza mahusiano yao.

Hata hivyo, alibainisha kwamba bado hawajabarikiwa na mtoto pamoja.

Stivo aliachana na mtumbuizaji Pritty Vishy mapema mwaka jana, miezi michache tu baada ya uhusiano wao kujulikana hadharani.

Wawili hao hata hivyo ilidaiwa hawakuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi kwani Stivo alidaiwa kutaka kusubiri ndoa kabla ya kushiriki tendo la ndoa na mtumbuizaji huyo mwenye umri wa miaka 21.