Uhasama kando, Alikiba ambariki kaka yake Abdukiba kufanya kazi na hasidi wake Diamond

Alikiba amesema kaka yake Abdukiba yuko huru kufanya kolabo na hasidi wake mkuu Diamond Platnumz

Muhtasari

• Alikiba alibainisha kuwa kaka yake ni msanii na yuko huru kufanya kazi na msanii yeyote anayetaka kufanya naye kazi.

•Mapema mwezi huu, Diamond Platnumz alifichua kuwa anafanyia kazi mradi mpya wa muziki na kaka yake Alikiba, AbduKiba

Abdukiba na kaka yake Alikiba
Image: INSTAGRAM

Staa wa muziki wa bongo, Alikiba amesema kaka yake Abdukiba yuko huru kufanya kolabo na hasidi wake mkuu Diamond Platnumz.

Wakati akihojiwa na waandishi wa habari siku ya Ijumaa jioni, Alikiba alibainisha kuwa kaka yake ni msanii na yuko huru kufanya kazi na msanii yeyote mwingine anayetaka kufanya naye kazi.

Kiba alisema ikiwa Abulkiba amefikia makubaliano ya kufanya kolabo na Diamond, basi wanaweza kuendelea na kushirikiana.

“Kama wameelewana wanafanya, wanafanya. Abdukiba ni msanii wa King’s, Diamond ni msanii wa Wasafi. Kwa hivyo, wanaweza kufanya,” Alikiba alisema.

Bosi huyo wa Kings Music Record hata hivyo alifichua kuwa Abdukiba bado hajawasilisha taarifa rasmi kwamba anafanyia kazi wimbo na mpinzani wake, Diamond Platnumz.

Licha ya hilo, Kiba hata hivyo aliweka wazi kuwa hana nia ya kumzuia kaka yake kufanya kazi na bosi huyo wa WCB.

“Ni wasanii, kila mtu anaweza akafanya kazi na kila mtu anayemtaka. Mtu yeyote anayemtaka, hilo halipinguki,” alisema.

Mapema mwezi huu, Diamond Platnumz alifichua kuwa anafanyia kazi mradi mpya wa muziki na kaka yake Alikiba, AbduKiba.

Diamond alitangaza hayo alipokuwa akizindua tamasha la Wasafi Festival ambalo aliwaalika bosi huyo wa Kings Music Records na mpinzani wake mwingine mkubwa Harmonize wa Konde Music Worldwide.

“Abdukiba (kaka yake Alikiba) atafanya collabo na mimi katika wimbo, nitakuwa naye kwenye tamasha na kaka yake Alikiba akiona inafaa, anaweza kuungana nasi, akitupa hata shoo moja tutashukuru. Harmonize pia, tunatakiwa kutumia akili zetu katika mambo haya, tusiweke mambo yetu binafsi kwenye haya mambo," alisema Diamond.

Huku akijibu mwaliko wa Diamond kwenye tamasha la Wasafi festival, Alikiba alibainisha kuwa hatakuwepo kwenye haflahiyo kwani atakuwa bize na mambo yake.

“Nipo bize na shughuli zangu,” alisema.

Diamond Platnumz na Alikiba wamekuwa wakizozana kwa muda mrefu sasa na mastaa hao wawili wa bongo fleva katika siku za nyuma wamewahi kuonyesha wazi mara nyingi uhusiano mbaya kati yao.