"Utazeeshwa na shida" Esther Musila awazima wanaosumbuliwa na tofauti ya umri kati yake na Guardian Angel

Musila amemzidi umri mume wake Guardian Angel kwa takriban miongo miwili.

Muhtasari

•Esther Musila ameendelea kuwasuta watu wanaopinga  ndoa yao na wale wanaowakosoa kuhusiana na tofauti kubwa ya umri kati yao.

•Bi Musila aliwasuta wanaosumbuliwa sana na tofauti zao za umri na kudokeza kuwa kila mtu atazeeka siku moja.

mnamo siku ya harusi yao Januari 2022.
Esther Musila na mumewe Guardian Angel mnamo siku ya harusi yao Januari 2022.
Image: INSTAGRAM

Mke wa mwanamuziki Guardian Angel, Esther Musila ameendelea kuwasuta watu wanaopinga  ndoa yao na wale wanaowakosoa kuhusiana na tofauti kubwa ya umri kati yao.

Musila ambaye amempiku umri Guardian Angel kwa takriban miongo miwili alifunga pingu za maisha na mwimbaji huyo wa nyimbo za injili mwanzoni mwa mwaka jana na wawili hao wamekuwa wakiishi pamoja kwa furaha. Hata hivyo, si kila mtu anafurahia ndoa yao kwani baadhi ya Wakenya wamekuwa wakikosoa muungano wao na kumkosoa kwa kuolewa na mwanamume ambaye ni mdogo zaidi yake.

Wakati akimjibu shabiki ambaye alikuwa akimuonyesha upendo na kuunga mkono ndoa yake kwenye Tiktok, mama huyo mwenye umri wa miaka 53 alibainisha kuwa wakosoaji wao wataendelea kuteseka kwa taabu na kwamba chuki yao haitaathiri ndoa yao kamwe.

“Wataendelea kuteseka katika masaibu yao. Chuki yao haijawahi na haitatubadilisha sisi ni nani, kwa hivyo hakuna kelele zozote zitakazotuzuia kuishi,” Bi Musila alisema.

Mama huyo wa watoto watatu wakubwa aliendelea zaidi kuwasuta wanaosumbuliwa sana na tofauti zao za umri na kudokeza kuwa kila mtu atazeeka siku moja.

"Umri ni sawia. Wewe unayejificha kwa pseudo hutazeeka?? Utazeeshwa na shida," Bi Musila alimjibu mkosoaji.

Tangu ajitose kwenye mahusiano na Guardian Angel takriban miaka mitatu iliyopita, Esther Musila ameshambuliwa mara nyingi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mahusiano hayo, hoja kuu ikiwa tofauti kubwa kati ya umri wao.

Mama huyo wa watoto watatu amemzidi umri Guardian Angel kwa takriban miongo miwili, jambo ambalo linafikiriwa kuwa si la kawaida katika jamii nyingi. Walakini, wanandoa hao wanaonekana kuridhika na kufurahia ndoa yao ya mwaka mmoja na mara nyingi wamekuwa wakiwakosoa wakosoaji wao na kuwathibitisha kuwa wako sawa pamoja.

Mwaka uliopita, mwanamuziki Guardian Angel aliweka wazi kuwa kupata watoto sio kipaumbele katika ndoa yake na Esther Musila.

Katika mahojiano ya Juni, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 34 alisema msingii kuu wa uhusiano wao ni mapenzi wala si watoto.

Guardian Angel alisema kwamba kupata mtoto na Bi Musila ni la ziada kutoka kwa Mungu  ambayo kwake si lazima wapate.

"Nilipoingia kwenye ndoa yetu, mtoto ni nambari mbili. Akija ama akose ni sawa. Nambari moja ni upendo wetu. Mungu akitaka kutupatia bonasi ya baraka ya mtoto ni sawa. Lakini kama haipo, hiyo ni bonasi, tunafurahia na tulicho nacho. Upendo wetu ndio ninaojali," Guardian alisema katika mahojiano na Plug TV.

Mwanamuziki huyo alisema upendo wao pekee umetosha na kueleza kuwa umemletea amani kubwa moyoni.

"Tukipata mtoto ni sawa, tukikosa pia haipunguzi chochote kwa upendo wangu kwa mke wangu," Alisema.

Wawili hao walifunga ndoa mnamo Januari 4 mwaka jana katika harusi ndogo iliyohudhuriwa na familia na marafiki wa karibu. Hii ilikuwa baada ya kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa zaidi ya mwaka mmoja.