Fahamu sababu tata ya Akothee kuzuiwa kuwahutubia wanafunzi wa Ng'iya Girls

Akothee amemsihi Askofu aliyefutilia mbali ziara yake kumwombea ili aweze kukutana naye mbinguni mnamo siku ya kiama.

Muhtasari

•Akothee alipaswa kuwa mgeni maalum wakati wa onyesho la talanta la shule hiyo na uzinduzi wa shughuli za hisani.

•"Kwa Askofu Mkuu ninaelewa unakotoka, endelea kutuombea sisi wenye dhambi, ili tukutane mbinguni siku hiyo," Akothee alisema.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amekubali kufutiliwa mbali kwa mwaliko wake katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Ng’iya, kaunti ya Siaya ambapo alikuwa amealikwa kuwahutubia wanafunzi.

Kulingana na barua ya mwaliko aliyoshiriki kwenye akaunti yake ya Instagram, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alipaswa kuwa mgeni maalum wakati wa onyesho la talanta la shule hiyo na uzinduzi wa shughuli za hisani.

“Shirika lako- Wakfu wa Akothee litatusaidia kufikia mashirika/kampuni zenye mawazo sawa ili kuunga mkono mpango huu. Tunategemea usaidizi wako ili kufanikisha uzinduzi huu. Pia unatarajiwa kutoa hotuba ya kutia moyo kwa wanafunzi kabla ya uzinduzi wa hisani kuanza,” barua ya mwaliko iliyoandikwa kwa Akothee ilisoma.

Mwanamuziki huyo asiyepungukiwa na drama katika maisha yake hata hivyo baadaye alipokea taarifa ya ujumbe kwenye mtandao wa WhatsApp ambapo alifahamishwa kuwa hakukaribishwa tena kwa mazungumzo na wanafunzi.

Katika ujumbe huo, mtumaji wa ujumbe alieleza kuwa askofu wa Kanisa la ACK katika eneo la shule hiyo hakuwa sawa na ziara yake.

“Habari ma’am. Tuna maendeleo mapya katika Ng'iya Girls. Tutaghairi hafla kwa sababu askofu wa ACK wa eneo hilo hafurahii uwepo wetu. Hata walienda shuleni na walikuwa wagumu sana kwa mwalimu mkuu, Madam Hellen,” ujumbe uliotumwa kwa Akothee ulisomeka.

Katika jibu lake kuhusu kughairiwa kwa hafla hiyo, mama huyo wa watoto watano alimshukuru mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Ngiya Girls, madam Hellen Juma kwa kufikiria kumwalika kuzungumza na wanafunzi wake licha ya kughairishwa kwa ziara yake.

Licha ya kuarifiwa kwamba hajakaribishwa shuleni, Akothee alimhakikishia mwalimu mkuu kwamba bado ataunga mkono juhudi zake za kuazisha wakfu wa kusaidia watu wasio na uwezo na alimtakia mafanikio katika mipango yake.

“Shule ya Upili ya Ngiya Girls sasa iko kwenye ramani, inayojulikana duniani kote, hata wale ambao hawakuwajua Ngiya Girls, sasa wanajua. Ninaomba kwamba maendeleo yako mapya ya kuwa na msingi ndani ya shule yatainua roho nyingi. Ninathamini sana upendo na imani uliyonayo kwangu. Bado nitaunga mkono kozi yoyote ambayo itaacha athari chanya kwa jamii yetu. Bado nitaunga mkono ninapoweza hata pale niliposimama.Mungu akubariki,” Akothee aliandika kwenye Instagram.

Mwimbaji huyo pia alikuwa na ujumbe kwa mtu wa Mungu ambaye alighairi ziara yake akisema, "Kwa Askofu Mkuu ninaelewa unakotoka, endelea kutuombea sisi wenye dhambi, ili tukutane mbinguni siku hiyo."

Sababu ya kughairiwa kwa ziara ya Akothee ilitokana na malalamishi ya wazazi, wahitimu wa shule hiyo ya wasichana, jumuiya na wadau wengine wahusika wa shule hiyo ambao walihisi kuwa mwanamuziki huyo haendani na wasifu wa mzungumzaji. 

Pia kulikuwa na malalamishi mtandaoni kutoka kwa kundi la Wakenya waliokuwa na maoni sawa kwamba yeye si mtu sahihi kuzungumza na vijana wadogo. 

Je, una maoni gani kuhusu Akothee kuwa mzungumzaji wa motisha kwa vijana? Tafadhali zungumza nasi kwenye sehemu ya maoni.