"Hatukula kitu!" Waimbaji wa ‘Kaveve Kazoze’ wafunguka masaibu yao baada ya wimbo wao kuvuma

Ngesh alisema kuwa anajisikia vibaya kuonekana kana kwamba ametajirika na muziki kumbe si kweli.

Muhtasari

•Bendi hiyo ililalamika hawakuvuna chochote kutokana na wimbo wao uliovuma nchini kwa kipindi kirefu mapema mwaka huu.

•Walidai kuwa zaidi ya umaarufu mkubwa, wimbo ‘Kaveve Kazoze’ uliovuma kwa muda mrefu haukuwa na manufaa makubwa ya kifedha kwao

Spider Clan
Image: HISANI

Kundi la muziki la Spider Clan, maarufu kwa wimbo wao wa Rieng Genje almaarufu Kaveve Kazoze wamejitokeza kufunguka kuhusu masaibu yao licha ya umaarufu mkubwa waliopata.

Katika mahojiano na Jalang’o TV, bendi hiyo ya wasanii wanne inayojumuisha ndugu na majirani kutoka kaunti ya Nyandarua ililalamika kuwa hawakuvuna chochote kutokana na wimbo wao uliovuma nchini kwa kipindi kirefu mapema mwaka huu.

Walidai kuwa hii ilisababishwa zaidi kwa sababu pesa nyingi zilizotolewa na wimbo kwenye YouTube zilienda kwenye akaunti ya mtayarishaji wa wimbo huo.

“Kwa ngoma ya Kaveve Kazoze hatukukulia kitu. Ilisimamiwa na mmiliki wa mdundo. Mwenye beat ndiye alikuwa anachukua hiyo pesa,” walisema

Wakaongeza, “Sasa wakati ngoma ilifikisha watazamaji milioni nne hapo ndio tumechanuka tukajua pesa inaweza kutokea kwake ije kwetu sasa.”

Walidai kuwa zaidi ya umaarufu mkubwa, wimbo wa ‘Kaveve Kazoze’ uliovuma kwa muda mrefu nchi nzima haukuwa na manufaa makubwa ya kifedha kwao.

“Kwa umaarufu, jina ni kubwa lakini pesa hakuna. Hadi ikifika ni kwenda shoo watu wanalia shida, eti uchumi ni ngumu,” walisema.

Huku akizungumzia jinsi maisha yalivyo baada ya wimbo wao kusambaa mitandaoni, Ngesh wa Vasha aliyeimba vesi maarufu ya ‘Kaveve Kazoze’ alisema kuwa anajisikia vibaya kuonekana kana kwamba ametajirika na muziki kumbe si kweli.

“Mtu huskia ako chini, unajua pale kwa mitandao ya watu walichachisha. Wakachachisha tuko na doh, tuko na doh lakini hatuna,” Ngesh alisema.

Aliongeza, “Mtu huskia tu ako down kwa sababu tukipatana na watu huku nje wanasema tuko na doh na huwezi mwambia huna pesa.”

Pia walilalamikia baadhi ya ahadi ambazo hazijatekelezwa ambazo walipewa na baadhi ya watu mashuhuri akiwemo mwanasiasa maarufu na kuwasihi watimize.