"Hawezi kusogeza mwili wake!" 2mbili atoa taarifa ya wasiwasi kuhusu afya ya Alpha Mwana Mtule

2mbili afichua kuwa Mwana Mtule amekuwa hapati wageni wa kumtembelea na anashindwa kabisa kuusogeza mwili wake.

Muhtasari

• 2mbili alifichua kuwa msanii huyo wa injili bado amelazwa katika Hospitali ya Kenyatta huku hali yake ya afya ikiwa mbaya.

•Mwana Mtule amekuwa akiugua kwa mwezi mmoja uliopita baada ya kudaiwa kulishwa sumu nyumbani kwa rafiki yake mwishoni mwa Oktoba.

Image: INSTAGRAM// 2mbili

Mchekeshaji 2mbili amewataka wasanii wenzake wa Kenya kujitokeza kwa wingi na kumuonyesha upendo na sapoti mwimbaji wa nyimbo za Injili Alpha Mwana Mtule ambaye anaugua.

Katika taarifa ya Jumanne jioni, 2mbili alifichua kwamba msanii huyo wa injili ambaye pia anajulikana kwa kuiga sauti ya mtangazaji DJ Afro bado amelazwa katika Hospitali ya Kenyatta.

Mchekeshaji huyo alifichua kuwa afya ya Mwana Mtule imeendelea kuzorota hasa baada ya wahudumu wa afya kudaiwa kuacha kumhudumia kutokana na bili kubwa ya hospitali isiyolipwa.

“Wasanii, vile vile tulikimbia kukula Pilau kwa Chef Maliha, tukimbie Pale KNH, tunampoteza Kaka, Sumu Inamuua polepole Wadi 10B Baada ya Hospitali Kusimama Kumhudumia kwa sababu Bili Yake Ni Kubwa. Na Hakuna Jitihada Zinafanywa. Ili Kuiangusha!” 2mbili alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aliambatanisha taarifa yake na picha yake akiwa amesimama kando ya kitanda cha hospitali aliyocholalia Mwana Mtule.

Mchekeshaji huyo alizidi kufichua kuwa Mwana Mtule amekuwa hapati wageni wa kumtembelea mara kwa mara na anashindwa kuusogeza mwili wake.

"Inasikitisha sana kwamba hakuna wageni hata watu ambao "walimuua"!! Hebu tumsaidie huyu Jamaa, nilikuwa KNH naye Leo, Hawezi kusogeza sehemu yoyote ya mwili wake! Tuma Chochote Ili Kumsaidia Paybill 891300 , Acc. 84711! KWA @mwanamtule,” alisema.

Mwana Mtule amekuwa akiugua kwa takriban mwezi mmoja uliopita baada ya kudaiwa kulishwa sumu nyumbani kwa rafiki yake mwishoni mwa Oktoba.

Takriban wiki mbili zilizopiya, ripoti ziliibuka mitandaoni kuwa mwimbaji huyo wa nyimbo za injili amelazwa akiwa mahututi.

Video ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha Mwana Mtule akiwa amelala kwenye kochi huku mwimbaji mwenzake B Classic akielezea hali yake mbaya.

“Wakenya wenzangu na wanamuziki, Alpha yuko katika hali mbaya na sasa hivi hawezi hata kuongea anajichafua hivyo, tunaomba msaada wa matibabu, haongei na hata hawezi kutembea," B Classic alisema kwenye video hiyo.

B Classic aliongeza kuwa walikuwa wakimpeleka hospitali na kwamba haikuwa kiki bali ni suala zito.

Mapema mwezi huu, Mwana Mtule alikanusha uvumi kuwa alijaribu kujitoa uhai akisema alilishwa sumu.

“Sijafa; Namshukuru Mungu kwa kuokoa maisha yangu. Nililishwa sumu kwa rafiki yangu Rongai. Nitazungumza hivi karibuni na kueleza kilichotokea kwa sababu sasa bado sijisikii vizuri… bado niko hai na polisi wanachunguza washukiwa,” Alpha alisema.

"Jameni, naumia sana nasoma comments watu wakisema…ni clout chasing tafadhali acheni, Ju ata saizi hali yangu sio nzuri vile mnafikiria, Nilipewa sumu sikujaribu kujitoa uhai" Mtule alisema.

“Nimeishi na Mungu wetu mitaani miaka tisa nikikula kwa taka taka Nilikua chokora pipa, sijawai ata fikiria kujiuwa, mbona nijaribu kuijiuwa wakati kama huu mungu Ananipanga,”

“Kipaji Mungu wetu Amenipea ni kubwa kushinda clout chasing, najua adui mnanitafuta kuniua ,nyi endeleeni tu MUNGU WETU haezi sahau Huyu Boyz 😞 #MIMI," Mwana Mtule alisema.