Hongera! Otile Brown ajawa bashasha akitangaza anatarajia mtoto wake wa kwanza

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30 aliahidi kumpa mtoto wake upendo wake wote.

Muhtasari

•"Bizeee hivi karibuni atakuwa papa, Inshallah.. Nitakupenda sana mtoto #Inshaallah," Otile Brown alisema.

•Mwanamuziki huyo mahiri hata hivyo hakufichua maelezo ya mzazi mwenzake au jinsia ya mtoto anayetarajia.

Msanii wa kizazi kipya Otile Brown katika mahojiano ndani ya rdio Jambo.
Msanii wa kizazi kipya Otile Brown katika mahojiano ndani ya rdio Jambo.
Image: Radio Jambo (Facebook)

Nyota wa muziki wa Kenya Jacob Obunga almaarufu Otile Brown ametangaza kuwa hivi karibuni atakuwa mzazi.

Katika taarifa yake siku ya Jumamosi jioni, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30 aliahidi kumpa mtoto wake upendo wake wote.

"Bizeee hivi karibuni atakuwa papa, Inshallah.. Nitakupenda sana mtoto #Inshaallah," Otile Brown alisema kupitia mtandao wa Instagram.

Mwanamuziki huyo mahiri hata hivyo hakufichua maelezo ya mzazi mwenzake au jinsia ya mtoto anayetarajia.

Tangu kutangaza utengano wake na mrembo wa Ethiopia, Nabayet mapema mwaka jana, Otile Brown amekuwa msiri  sana kuhusu mahusiano yake.

Mwimbaji huyo alichumbiana na Nabayet kwa takriban miaka minne kabla ya kutangaza kutengana kwao mwaka jana. Kabla ya kujitosa kwenye mahusiano na mrembo huyo wa Ethiopia alichumbiana na Vera Sidika.

Wakati akichumbiana na Vera Sidika miaka  kadhaa iliyopita, Otile Brown alidaiwa kumtunga mimba mwanasosholaiti huyo .

Mama huyo wa watoto wawili hata hivyo alidaiwa kutoa ujauzito huo, madai ambayo mara nyingi ameyatupilia mbali.

Wakati akiwashirikisha wafuasi wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram  mapema mwaka huu, shabiki mmoja alimtaka mwanasosholaiti huyo ajibu madai kwamba alitoa ujauzito wa Otile Brown wakati wa mahusiano yao.

"Ni kweli ulitoa mimba ya mtoto wa Otile Brown?" shabiki aliuliza.

Katika jibu lake, mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 33 alibainisha kuwa hakuwahi kuwa mjamzito wakati wa mahusiano yake na Otile Brown. Pia aliweka wazi kuwa kamwe hawezi kutoa mimba.

"Unawezaje kutoa mimba ambayo haikuwahi kuwepo? Kusema kweli, siwezi kufanya biashara hii. Ninapenda watoto sana. Ninaweza kupat 10 kama ningeweza," alisema.

Katika wimbo wake 'Niacheni' ambao aliachia miaka kadhaa iliyopita, mwimbaji Otile Brown alidokeza kuwa alitoka kwenye mahusiano fulani baada ya mwanamke aliyekuwa akichumbiana naye kutoa mimba.

Mashabiki wake waliamini alimzungumzia Vera Sidika katika wimbo huo wa hisia alioutoa baada ya kutengana kwao.

“Usijifanye eti hujui, Tatizo mimba yangu ulioitoa, Mimi niacheni msione nipo kimya mwenzangu nina mengi. Wacha nilie na moyo wangu maneno maneno mimi sipendi. Nitafanya vizuri zaidi", Otile aliimba.