"Kwa Mathe tumefunga!" DCI wawaagiza wateja wa mihadarati kutafuta muuzaji mwingine

“Kwa Mathe tumefunga. Tafuteni pedi mwingine,” DCI walitangaza.

Muhtasari

•DCI waliwataka wateja waliokuwa wakitembelea eneo hilo kwa ajili ya kununua mihadarati kutafuta muuzaji mwingine.

•Jumanne, washukiwa 4 walikamatwa baada ya shehena kubwa ya bangi na shilingi milioni 13.4 pesa taslimu kupatikana katika mtaa wa Ngara.

Image: HISANI

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) mnamo siku ya Jumatano ilitangaza kwa utani kufungwa kwa eneo maarufu la uuzaji wa dawa za kulevya katika mtaa wa Ngara maarufu kama ‘Kwa Mathe.’ 

Katika taarifa fupi kwenye mitandao ya kijamii, wapelelezi hao waliwataka wateja waliokuwa wakitembelea eneo hilo kwa ajili ya kununua mihadarati kutafuta muuzaji mwingine.

“Kwa Mathe tumefunga. Tafuteni pedi mwingine,” DCI walitangaza kwenye mtandao wa Facebook.

Taarifa hiyo iliambatanishwa na picha ya ramani ya  ‘Kwa Mathe’ ambako kunaaminika kuwa eneo la kuuzwa na dawa za kulevya.

Siku ya Jumanne, idara hiyo iliripoti kukamatwa kwa washukiwa 4 baada ya shehena kubwa ya bangi na shilingi milioni 13.4 pesa taslimu kupatikana katika mitaa ya mabanda ya Kariua, mtaa wa Ngara, jijini Nairobi.

Teresia Wanjiru na vijana watatu wadogo wenye umri wa kati ya miaka 16 na 17 walitiwa mbaroni kwa mahojiano zaidi kufuatia operesheni hiyo na walitarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumatano.

Washukiwa hao walikamatwa katika eneo la uhalifu wakati wa operesheni ambayo iliendeshwa na wapelelezi kutoka Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya na Kitengo cha Kitengo cha Uhalifu Uliopangwa wa Kimataifa kwa usaidizi wa Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi kutoka Parklands ambao walivamia eneo hilo kufuatia taarifa za kijasusi.

Baadhi ya vitu zilizopatikana katika operesheni hiyo ya Jumanne ni pamoja na mifuko miwili iliyokuwa na mamilioni ya pesa zilizofichwa ndani yake, mifuko 26 ya bangi, katoni 4 za karatasi za kusokota, peremende 173 zilizopakiwa na katoni ya vitafunio vinavyoshukiwa kuwa ‘weed cookies.’

Kufuatia kukamatwa kwa wanne hao, mitandao ya kijamii ilishika moto huku wanamitandao Wakenya wakidai kuwa mwanamke aliyekamatwa, Bi Teresia Wanjiru ni muuza madawa ya kulevya maarufu, ‘Mathe wa Ngara.

Chini ya taarifa ya kukamatwa kwa Bi Teresia, mtumizi wa twitter aliwajibu akiwafahamisha kuwa licha ya kudaiwa kumkamata ‘Mathe’, hawawezi kulifunga eneo maarufu ambalo alifanyia biashara, ‘Kwa Mathe.’

"Mnaweza kumkamata mathe lakini huwezi kumkamata kwa mathe," @iamgrande aliandika.

Katika jibu lao, wapelelezi hao walithubutu mtumiaji huyo wa Twitter kujitokeza katika eneo hilo maarufu bila silaha.

“Sawa. Tupatane kwa mathe. Na mtu asije na mawe,” DCI walijibu.

Image: FACEBOOK// DCI