Eddy Kenzo azimia baada ya kutajwa kuwania tuzo za Grammy

Katika video, msanii Eddy Kezno alianguka chini na kuzimia alipoona jina lake limetajwa kuwa miongoni mwa wawaniaji tuzo hizo maarufu duniani.

Muhtasari

• Kenzo alitangazwa kuwania katika kipengele cha Best Global Music Performance, ngoma yake ikiwa ni Give Me Love aliyomshirikisha msanii Matt B.

Msanii wa Uganda, Eddy Kenzo
Msanii wa Uganda, Eddy Kenzo
Image: Instagram//Eddy kenzo

Hivi tatizo ni lipi muziki wa wasanii wa Kenya hawatusi kimataifa? Hili ni swali ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiulizwa na litazidi kutanda katika vichwa vya wadau wengi wa muziki wa Kenya.

Wakati Wakenya wanazidi kukuna vichwa wasipate jibu la hili, wasanii kutoka mataifa jirani wanazidi kung’aa na kuzikwea ngazi za mafanikio kimuziki si tu katika ukanda wa Afrika Mashariki bali hata kutambulika kote ulimwenguni.

Mwezi mmoja baada ya wasanii mbalimbali kutoka taifa jirani la Tanzania kutangazwa kujumuishwa kwenye orodha ya wasanii wa kuwania vipengele mbalimbali katika tuzo za AFRIMMA na MTV, usiku wa kuamkia Jumatano ilikuwa zamu ya msanii Eddy Kenzo kutoka Uganda kutangazwa kuwania tuzo maarufu kabisa duniani – Grammy!

Msanii huyo mkali wa ‘Stya Loss’ alikuwa na mashabiki wake katika ukumbi mmoja ambapo walikuwa wanatizama runinga orodha ya wasanii wawaniaji ikitangazwa moja kwa moja.

Alirekodi tukio hilo na kulipakia kwenye Instagram yake ambapo alisema ni furaha na alfajiri mpya kwa muziki wa Afrika Mashariki kwani yeye ndiye msanii wa kwanza kutoka ukanda huo kuteuliwa kuwania tuzo za Grammy.

Kenzo alitangazwa kuwania katika kipengele cha Best Global Music Performance, ngoma yake ikiwa ni Give Me Love aliyomshirikisha msanii Matt B.

“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa wakati huu mzuri katika nchi yetu 🇺🇬. Ndugu yangu @mattbworld asante kwa kuwa na kipaji kikubwa sana. @gscelsa @angelavbenson @steynmusic asante kwa rekodi hii. Msanii mwenzangu nataka kukushukuru, hii ni yetu sote. Na kwa nchi ya mama yangu Uganda 🇺🇬 asante kwa kunilea. Tupo kwenye #Grammys @recordingacademy” Eddy Kenzo aliandika kwenye video hiyo akishangilia kwa furaha.