Pastor Ezekiel atetea hatua yake ya kuwauzia waumini 'maji ya hai' badala ya kuwapa bure

Mchungaji huyo huwa anawauzia waumini wake maji na vitambaa vya hanchifu vyenye nembo ya kanisa lake.

Muhtasari

• Alisisitiza kuwa watu kujaa uwanja wa Kasarani haikuwa nguvu yake bali uwepo wa Mungu.

• Ezekeil huwa anawauzia waumini wake maji na hanchifu kwa shilingi 100 za Kenya.

mchungaji Ezekiel Odero
mchungaji Ezekiel Odero
Image: Facebook

Mchungaji Ezekiel Odero kutoka kanisa la New Life ambaye aligonga vichwa vya habari hivi majuzi baada ya umati wa waumini kujaza uwanja wa Kasarani  ametetea hatua yake ya kuwauzia waumini wake maji yaliyo hai na vitu vingine.

Kupitia mahojiano ya kipekee na jarida la Daily Nation, Odero alisema kuwa maji hayo pamoja na vitambaa vya kupenga makamasi vimefanikisha huduma yake ya uponyaji kwani tayari zaidi ya waumini elfu 5 wanaoamini na kuvitumiqa wamepokea uponyaji.

Odero alisema kuwa vitambaa hivyo na maji ‘hai’ anauza kwa waumini wake kwa shilingi 100 na ili kuzuia ulaghai, huwa vinakuwa na chapa ya nembo za kipekee za kanisa lake.

“Iwapo watu watanunua na kutumia vitu hivyo kutoka kwa walaghai na kushindwa matarajio yao, mimi ndiye nitabeba lawama.”

Alisema hakuna kitu kinachofanya bihaa zake kuwa za kipekee kutokana na vingine bali ni maombi na Imani tu, huku pia akisema Imani hiyo ndiyo ilimfanya kuvutia umati mkubwa katika uwanja wa Kasarani.

“Hakuna kitu maalum katika chupa. Ni maji yaliyotakaswa. Ninaiombea. Nguo zilizotumiwa na Paulo katika Biblia ziliponya watu wengi. Vivuli vya manabii pia vilikuwa na nguvu za uponyaji. Tunapoomba, ni nguvu za Mungu zinazoponya. Mungu huwapa wachungaji nguvu. Mimi ni mwanadamu na Mungu atabaki kuwa Mungu,” mchungaji Ezekiel alisema.

Alitetea hatua yake ya kuuza bidhaa hizo kwa waumini kinyume na dhana ya wengi kuwa anafaa kuwapatia bure. Alisema pesa hizo ndizo anatumia kununua zingine, kuzipiga chapa na kuzitakaza kabla ya kuwauzia waumini.