Dennis Okari kujiunga na Mark Masai katika podcast kwenye mitandao yao ya kijamii

Alisema podcast hiyo itakuwa inahusu hadithi za watu wengi waliowaboreshea maisha.

Muhtasari

• Okari na Masai wote waliondoka NTV wiki jana baada ya kuhudumu kwa miaka kadhaa kama wanahabari.

Wanahabari Mark Masai na Dennis Okari
Wanahabari Mark Masai na Dennis Okari
Image: Facebook

Mtangazaji Dennis Okari aliyepoteza kazi katika kituo cha runinga cha NTV amefichua kuwa atakuwa anashirikiana na mwenzake Mark Masai katika podcast yake mpya ya The Social Newsroom kwenye mitandao ya kijamii.

Okari na Masai walipoteza kazi zao wakati mmoja hivi majuzi katika kituo cha NTV na wote sasa wameamua kuendeleza urafiki wao nje ya kampuni hiyo kwa kufanya podcast ya pamoja.

Podcast hiyo itazinduliwa Alhmanisi jioni kulingana na maneno ya Masai ambaye alieleza mapema wiki hii.

“Mabibi na Mabwana: Hapa ni kwetu! Kwa njia mpya ya kufanya mambo. Ili kupata maana katika yale tunayopitia. Ili kupata hadithi ambazo ni muhimu kwetu. Karibu kwa mwelekeo wa mustakabali. #TheSocialNewsoom na @semaboxAfrica Tiririsha Alhamisi hii saa kumi na mbili jioni kwenye mitandao yangu ya kijamii. Kama kawaida, Sambaza, mwambie rafiki!” Masai aliandika.

Okari pia alitangaza kwenye Twitter yake akisema kuwa katika podcast hiyo, watakuwa wanazungumzia maisha yao na ya wale ambao wamewafanya kuwa watu wa kujinafasi kijamii.

“Hapa kuna hadithi nyingi na watu ambao wameboresha maisha yetu. Kwa hadithi zaidi na mabadiliko ya kusisimua! Salamu! Ungana nami Alhamisi hii, Moja kwa moja kwenye kurasa zangu zote na @markmasai na @semabox,” Okari alisema.

Wiki moja iliyopita wakati wa kuondoka NTV, Okari aliandika ujumbe wa kuwashukuru waajiri wake na pia Mungu akisema kuwa Muda wake wa kuhudumu pale ulikuwa umefikia kikomo.

“Mgawo wangu katika NTV umefika mwisho. Ninamshukuru Mungu kwa nafasi ya kutumikia. Nilitoa yote yangu. Nisingeweza kufanya hivyo bila msaada wa timu ya ajabu na watazamaji wa ajabu. Ni wakati wa kuendelea na jambo kubwa na kubwa kuliko mimi,” Okari alisema.