Mwanamuziki wa injili anayeugua Fistula avalia nepi hadharani ili kuhamasisha umma

Alivutia umati mkubwa wa watu huku wakazi wakitafuta kujua kwa nini alikuwa akivaa nepi.

Muhtasari
  • Mwimbaji huyo aliyevalia kofia ya baba Krismasi pia alienda katika soko la wazi la Eldoret Magharibi kwa ajili ya kuhamasisha
mWIMBAJI WA NYIMBO ZA INJILI WILLIAM GETUMBE
Image: MATHEWS NDANYI

Mwanamuziki wa nyimbo za injili William Getumbe alizua taharuki mjini Eldoret alipovaa nepi na kucheza barabarani ili kuhamasisha umma kuhusu magonjwa ya saratani, Fistula na maradhi mengine ya mtindo wa maisha.

Getumbe anasumbuliwa na tatizo la fistula kwa wanaume hali ambayo imemlazimu kuvaa diappers kila mara.

Mwimbaji huyo aliyevalia kofia ya baba Krismasi pia alienda katika soko la wazi la Eldoret Magharibi kwa ajili ya kuhamasisha.

Alivutia umati mkubwa wa watu huku wakazi wakitafuta kujua kwa nini alikuwa akivaa nepi.

Alieleza kuwa kwa miaka kadhaa amekuwa akisumbuliwa na tatizo la kutokwa na mkojo bila breki na kumlazimisha kuvaa nepi.

"Niliamua kujitokeza na kutumia hali yangu kuhamasisha umma kwa sababu najua kuna watu wengi wanasumbuliwa na hali hiyo lakini wanateseka kimyakimya badala ya kujitokeza kuzungumza na kusaidiwa", Getumbe alisema.

Getumbe ambaye ni baba wa watoto wawili alisema amezungumza na mkewe na watoto wake ambao wamekubali hali yake.

"Kuna wale ambao hawataki kuongea na wametelekezwa na familia zao na jamii bado wanaweza kusaidiwa kupata matibabu au msaada mwingine wowote", Alisema.

Alisema pia alikuwa akitumia muziki wake wa injili na mahubiri ya makanisa kuhamasisha Wakenya kuhusu magonjwa hayo.

Aliitaka serikali kuimarisha mfumo wa afya na kuzingatia magonjwa hayo au matatizo ya kiafya ambayo huathiri watu wengi

“Tunamsihi Rais ahakikishe kuwa vitu kama vile vitambaa ni nafuu ili viweze kufikiwa kwa urahisi na sisi tunaosumbuliwa na fistula”, Getumbe alisema.

Duncan Arum kutoka Unity Love Foundation alisema wameshirikiana na Getumbe kusaidia shughuli za uhamasishaji.

"Tuliamua kuungana naye kwa sababu kupitia taasisi hiyo tumerekodi visa vingi vya wanaume wanaougua kimyakimya kutokana na magonjwa kama vile fistula", Arum alisema.

Aliwataka Wakenya walio na changamoto kama hizo kujitokeza na kuzungumza ili wapate usaidizi unaohitajika,” Arum alisema.

Arum alisema watapeleka kampeni za uhamasishaji katika maeneo mengine nchini.