Mwanamuziki Madonna amsifia muasisi wa SHOFCO kwa kuwasaidia watu maskini Kibera

Madonna alikutana na Kennedy Odede, mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la SHOFCO katika mtaa duni wa Kibera, Nairobi.

Muhtasari

• Madonna alizuru Kenya siku kadhaa baada ya kuzuru Malawi ambapo amezuru shirika la Raising Malawi ambalo pia linafanya kazi sawia na ya Shofco.

Madonna afurahia mandhari ya Kibera
Madonna afurahia mandhari ya Kibera
Image: Instagram

Mwanamuziki Mmarekani Madonna ambaye tangu mwishoni mwa mwaka jana amekuwa katika ziara ya Krismasi barani Afrika alizuru mtaa wa mabanda wa Kibera jijini Nairobi na kujumuika na watoto waliofurahia kukutana naye.

Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 64 licha ya kuonekana mbichi alifurahia kazi ya Kennedy Odede, muasisi wa shirika lisilo la Kiserikali la SHOFCO ambalo hutoa huduma mbalimbali kwa watu vwa mitaa ya kimaskini nchini Kenya.

Madonna alimsifia Odede kwa juhudi zake za kutoa huduma katika mitaa kama Kibera ikiwemo ni vyakula, elimu na maji kwa watu hao ambao hawana uwezo wa kumudu bidhaa hizo za kimsingi katika maisha.

“Watoto wangu waliunda kinyago cha vioo vilivyovunjika huko Kibera kwa heshima ya kazi kubwa ambayo Kennedy Odede — anafanya @shofco, Shirika alilounda Alipokuwa mtoto akiishi katika vitongoji duni vya Nairobi ili kuboresha maisha ya familia Zinazoishi katika hali hizi zenye changamoto. Kuzingatia kuchuja maji, Elimu, Uwezeshaji wa mikopo kwa wanawake na wanaume kuanzisha biashara na kukomesha ukatili wa kijinsia Kwa kuwawezesha wanawake, kuchukua hatua za kisheria na kuwapa nafasi salama ya Kujenga Upya maisha yao,” Madonna alisema.

“Tumefurahishwa sana na kazi yake na kujitolea kwake kwa Jumuiya hii na tunafurahi kuendelea kufanya kazi naye na mkewe Jessica.”

Mwanamke huyo amedumu kwenye tasnia ya muziki wa Pop mpaka kubandikwa kwa jina Malkia wa Pop na mashabiki wake na kwa miaka mingi amekuwa akitumia nafasi yake katika jamii kuendeleza vita dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia miongoni mwa mmaswala mengine yanayokumba watu kijamii.