Prince Harry: Ndugu yangu William alinipiga na kunitupa kwa sahani ya mbwa

Harry alisema kuwa William alikuwa anamuita mkewe Meghan kuwa mkaidi na mgumu kuelewa.

Muhtasari

• “William alinishika kwa nguvu kola ya shati, akararua tai yangu na kuniangusha chini kwa sahani ya mbwa,” Prince Harry alinukuliwa na majarida ya Uingereza.

Prince Harry asema nduguye Prince William alimpiga 2019
Prince Harry asema nduguye Prince William alimpiga 2019
Image: US Weekly

Vita katika kasri la kifalme ya Buckingham nchini Uingereza kati ya watoto wa kifalme Prince Harry na kakake mkubwa Prince William vinaendelea kuchukua mkondo tofauti.

Hii ni baada ya  Prince Hary ambaye alijiondoa katika familia hiyo ya kifalme kudai kuwa William alimshambulia mwaka 2019 na kumpiga vibaya sana kabla ya kumtupa kwenye sinia ya chakula cha mbwa.

Katika kionjo cha mahojiano ambayo yamesambaa kote ulimwenguni, Harry alielezea kwamab zogo baina yake na kakake lilianza wakati Prince William alimuita mke wa Prince Harry, Meghan kuwa ni mtu mkaidi na mgumu kueleweka.

Hapo ndipo Harry alijaribu kuingilia kati lakini ndugu yake akamgeuzia kibao kwa kumshika kwa nguvu kwenye kola ya shati, akamvuta na kumuangusha kweney sahani ya mbwa.

Kionjo hicho ambacho kilivujishwa ni kutokana na tawasifu ya Harry ambayo inatarajiwa kuzinduliwa siku chache zijazo na hilo ni tukio moja ambalo alilizungumzia na kulieleza kama shambulizi la kimwili kutoka kwa ndugu yake.

“William alinishika kwa nguvu kola ya shati, akararua tai yangu na kuniangusha chini kwa sahani ya mbwa,” Prince Harry alinukuliwa na majarida ya Uingereza.

Kwa zaidi ya miaka 3 sasa, Prince Harry hajakuwa na uhusiano mzuri na wanafamilia yake ya Kifalme katika kasri la Buckingham tangu alipofunga ndoa na Meghan Markle, mwanadada Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika.

Wawili hao walijiondoa kutoka kwa familia ya kifalme na kuenda zao Marekani kuanza maisha yao binafsi katika kile majarida yaliripoti kuwa Meghan alikuwa akinyanyapaliwa na kubaguliwa kutokana na rangi ya ngozi yake.

Madai hayo yalikanushwa vikali na Malkia Elizabeth wa pili kipindi hicho akiwa hai lakini vyanzo vingi vya habari viliripoti kuwepo kwa suala la ubaguzi wa rangi katika familia hiyo.