Magix Enga akiri hayuko sawa, aomba radhi kwa aliyemkosea kumfanya awe duni

Mwishoni mwa mwaka jana, Enga alionekana Pwani ya Kenya akiwa katika hali duni ambayo si ya kawaida.

Muhtasari

•Enga alikiri kuwa japo kipaji bado kipo, lakini haoni mambo yake yakienda kama kawaida huku akihisi kuna mkono wa mtu katika hilo.

Mzalishaji wa muziki Magix Enga akiri hayuko sawa
Mzalishaji wa muziki Magix Enga akiri hayuko sawa
Image: Facebook

Mzalishaji na ambaye ni mwanzilishi wa midundo ya Gengetone nchini Kenya, Magix Enga amekiri wazi kuwa mambo yake hayaendi sawa hata kama bado kipaji kipo.

Enga anahisi kukwama kwa mambo yake si jambo la kawaida na pengine kuna mkono wa mtu unahusika.

Magix Enga ambaye alivuma sana kati ya mwaka 2018 na 2020 kama produsa wa midundo ya gengetone na pia msanii wa ngoma hizo, kwa muda mrefu sasa amekuwa akionekana katika hali isiyo ya kawaida, baadhi wakihisi huenda anasumbuliwa na tatizo la msongo wa akili na pengine unyongovu.

Katika ujumbe mfupi na wenye ukakasi mkubwa ambao alichapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook, Enga alisema kuwa pahali amefikia hata yeye mwenyewe haelewi kitu chochote ila akaahidi kuwa bado anawakubali sana mashabiki wake na wote wanaojitoa zaidi kwa ajili ya kumjulia hali.

Alifuchua kuwa anapitia mtihani mgumu sana katika maisha yake na kukiri huwa japo talanta ya kuimba na kuunda midundo bado iko lakini haelewi mbona mambo yake yamekwama.

“Habari watu wangu 🙏🏿 pahali maisha yamenifikisha sielewi chochote ️ nawapenda sana. Talanta Iko japo siko poa. Napitia mambo mengi sana na sielewi mbona 😔 mtu yeyote tafadhali. Kama nilikosea naomba radhi. Upendo zaidi kwenu nyote,” Enga aliandika.

Produsa huyo alisemekana kuzalisha na kupalilia uhasama baina yake na produsa mwingine kwa jina Motif ambaye pia ni mwanzilishi wa midundo ya gengetone.

Mwishoni mwa mwaka jana, Magix Enga alionekana katika kaunti ya Kilifi akiwa katika hali ya kutamausha ambapo video na picha zilizoenezwa mitandaoni zilimuonesha akiwa chini ya mti, miguu peku, nguo zilizochanika na nywele chafu zilizokuwa katika hali duni ajabu.

Wengi wamekuwa wakimuombea kurejea katika hali yake ya kawaida na kurudisha maisha yake, baadhi wakidai kuwa huenda alizamia matumizi ya dawa za kulevya kama teja.