Nana Owiti aonesha furaha yake rapa Quincher Kanambo akiingia kidato cha 2

Alimtaka rapa huyo kutochanganywa na mawazo na mwanawe kwani watampa malezi anayostahili.

Muhtasari

• King Kaka na mkewe Nana Owiti walimrudisha Kanambo shuleni mwaka jana baada ya kuachia shule njiani miaka kadhaa iliyopita alipopata mtoto.

Nana Owiti na Quincher Kanambo Dede
Nana Owiti na Quincher Kanambo Dede
Image: InstaGRAM

Mtangazaji wa runinga ambaye pia ni mke wa mwanamuziki King Kaka, Nana Owiti ameonesha furaha yake kwa hatua za kimasomo anazozipiga rapa Quincher Kanambo ambaye familia hiyo ilimrudisha shule.

Kanambo ni msanii aliyetambulika mwaka jana baada ya klipu yake akichana mistari kusambazwa hadi kumfikia King Kaka, Msanii huyo aliamua kumpa nafasi ya kuendeleza kipaji chake kwa kumwaliko studioni na kumpa fursa ya kurekodi ngoma moja.

Baadae Kanambo aliwaelezea safari yake ya maisha na jinsi alilazimika kuachia shule njiani, hadithi iliyowagusa. Waliamua kumrudisha shule na kufadhili masomo yake baada ya msichana huyo kuridhia pendekezo hilo.

Alirudi shuleni na kuanzia kidato cha kwanza na sasa Nana Owiti kipindi hiki ambapo watoto wanarudi shule, alifurahia na kudokeza kuwa alikuwa anaingia kidato cha pili.

“Majukumu ya mama. Ni msimu wa kurudi shuleni kwa mtoto wetu mwingine mkubwa @quinchermkanambo. Anajiunga na kidato cha 2 jamani! Ninajivunia sana ukuaji wake wa pande zote. Tunapoketi kwenye maegesho, ananiambia kuhusu ndoto zake. Ni KUBWA SANA. Ninamkumbusha kuwa kuwa na ndoto ni vizuri lakini wapangaji wana uwezo wa juu. Anatikisa kichwa kwa uthibitisho mwingi,” Nana Owiti alisema.

Pia alisimulia jinsi amekuwa akimhimiza kuzingatia masomo na kutochanganywa na fikira za mwanawe mdogo ambaye anaishi na familia hiyo.

Ikumbukwe katika wimbo wake wa kwanza, Kanambo alijieleza kwa mapana kuwa alilazimika kuacha shule baada ya kupata ujauzito wa mwanawe huyo wa kiume.

Owiti alimhakikishia kuwa mtoto wake watampa malezi yote anayostahili huku akimtaka rapa huyo kujikita zaidi vitabuni.

“Ni mtu mweney maono maubwa na najua shida pia na hivyo namkumbusha asiwe na wasiwasi na mambo ambayo hawezi kuyabadilisha kwa sasa na hiyo ni pamoja na kutofikiria kupita kiasi kuhusu Lonje(mwanawe) au mtu yeyote kwa jambo hilo bali kulifunika tu katika maombi na kumwachia Mungu,” Nana alidokeza ushauri wake kwa Kanambo.