Rayvanny ampokonya Harmonize 'mpenzi' wake mpya, amchezea gitaa kwenye kochi

Rayvanny alionekana akiwa na mrembo huyo kwenye kochi huku akimchezea gitaa, huku mrembo anapiga mafunda ya maji kwenye gilasi.

Muhtasari

• Mrembo huyo alionekana mara ya kwanza wiki tatu zilizopita na msanii Harmonize wiki tatu zilizpopita wakiwa katika hali ya ukakasi.

Rayvanny aonekana na mrembo wa Harmonize
Rayvanny aonekana na mrembo wa Harmonize
Image: Instagram

Msanii Rayvanny kutoka lebo ya Next Level Music amegonga vichwa vya habari baada ya kuonekana akimchezea gitaa mrembo Feza Kessy ambaye alionekana na Harmonize wiki tatu zilizopita.

Feza Kessy ambaye alishiriki kama vixen kwenye video ya ngoma ya Wote iliyoachiwa na Harmonize wiki tatu zilizopita aliibua madai kuwa huenda ni mpenzi mpya wa msanii huyo wa Konde Music Worldwide, haswa baada ya kudaiwa kuachwa na Fridah Kajala Masanja.

Uvumi huo ulikolezwa munyu pale ambapo Feza kwenye moja ya chapisho lake la Instagram alijitambulisha kama Feza Konde, akitumia jina la Harmonize la Konde Boy.

Watu kadhaa waliwamiminia sifa Feza na Harmonize wakidai kuwa wanaendana sana kama wapenzi, jambo ambalo Harmonize alikubali na kusema kuwa watu wengi wamemwambia wanaendana na Feza.

Lakini tangu kuachia video ya ‘Wote’ Feza ndio hivyo alipotea tena hakuwahi onekana katika mizunguko ya Harmonize.

Safari hii ameibukia kwake Rayvanny ambapo walionekana wamebatrizi juu ya kochi moja la kistarehe, ambapo Rayvanny alidokeza ni studioni.

Msanii huyo alikuwa anamchezea Kessy ngoma na gitaa mkononi huku mrembo akicheka na kutokwa na tabasamu kubwa mpaka jino la mwisho kuonekana.

Sasa haijajulikana iwapo mrembo huyo ako kwa Rayvanny kwa ajili ya mradi wa kushiriki kwenye ngoma yake ijayo kama vixen ama ndio yale yale tena ya kusemwa kuwa ameingia kimapenzi  na Vanny Boy.

Feza kuonekana kama anawagonganisha Rayvanny na Harmonize ni hadithi kubwa kwani wasanii hao wawili ambao awali walikuwa marafiki chini ya lebo ya WCB Wasafi, sasa hivi ni maadui ambao hawawezi kupikwa katika jungu moja.

Hivi majuzi, walichafuana mitandaoni kwa maneno ya nguoni pale ambapo Harmonize aliotesha ugomvi kwa kutupa mkwara kwa Rayvanny dhidi ya kutoa wimbo wenye maudhui ya pombe, akilenga wimbo wake wa Nitongoze.