Diamond kuachia wimbo wa 4 chini ya wiki mbili, "Ni mwaka wa vyuma juu ya nonda!"

Alisema wimbo wake wa Zuwena hajaufanyia promosheni yoyote lakini bado unazidi kutamba.

Muhtasari

• Mpaka sasa chini ya siku 14, msanii huyo ameachia ngoma tatu, akiendeleza ahadi yake kuwa huu mwaka ni ngoma tu atakuwa akitoa.

Diamond Platnumz
Diamond Platnumz
Image: Instagram

Msanii namba moja katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa muda wote Diamond Platnumz amewamiminia sifa tele mashabiki wake kwa kumuonesha upendo mkubwa katika ngoma zake tatu ambazo ameziachia kwa mfululizo chini ya mwezi mmoja uliopita.

Platnumz alisema kuwa si rahisi kwa msanii kuachia ngoma kwa mfululizo na kukaa kimya pasi na kuzisukuma kupitia mitandao yake ya kijamii ili kufikia mashabiki, lakini mashabiki hao hao bila hata kutaarifiwa bado wanajitoa pakubwa kuzipakua na kuzifanya ngoma hizo kuwa pendwa.

“Inahitaji nguvu, Baraka, upendo mkubwa na sapoti kubwa kutoka kwa watu kutoa wimbo na kukaa siku tatu haujapakia kwenye mitandao wala kufanya challenge mbele ili kusukuma wimbo huo lakini bado ukakubalika, halafu kila siku wimbo ukazidi kufanya vyema,” Platnumz alisema.

Alisema yeye kutamba bila kufanyia wimbo promosheni ni ishara kubwa sana kutoka kwa mashabiki huku akisisitiza ahadi yake yam waka huu kwamba ni mwaka wa kutoa nyimbo baada ya nyimbo mfululizo hadi mashabiki wake wajivunie kumfuatilia.

“Hakika mashabiki wangu mnanipa faraja sana, nyinyi ni Zaidi ya mashabiki kwangu. Nyinyi ni familia yangu na nawashukuru kwa sapoti yenu, upendo na jema mlitendalo kwangu. Vyote naviona na niwaambie mashine nyingine iko njiani. Kama nilivyowaahidi, huu ni mwaka wa vyuma juu ya nonda,” Diamond alisisitiza.

Msanii huyo amekuwa akiporomosha ngoma baada ya ngoma katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, jambo ambalo limewafanya baadhi ya mashabiki na washikadau wa muziki kuhisi kuna mtu alimkosea na anataka kulipa kisasi kwa kuchomoa madude mazito mfululuzo.

Chini ya wiki mbili zilizopita, Diamond ameachia ngoma tatu zikiwemo, Yatapita, Zuwena na My Baby na sasa ametangaza kuachia dude la nne hivi karibuni kabla hata watu kuchoka na hizo tatu.

Mapema wiki hii meneja wake Babu Tale alifichua kwamba ngoma ya Zuwena iliandikwa miaka 4 iliyopita na kufichua pia kuwa kuna ngoma zingine mbili zitatoka hivi karibuni na ambazo ziliandikwa na msanii huyo miaka 7 iliyopita.