Msanii wa Afrika Kusini rafiki wa Diamond, AKA auawa kwa kupigwa risasi

Msanii huyo alipigwa risasi 6 nje ya mgahawa alikokuwa anajiandaa kutumbuiza usiku wa Ijumaa.

Muhtasari

• Taarifa zilisema msanii huyo alikuwa na mwenzake nje ya kilabu wakijiandaa kutumbuiza kabla ya tukio kujiri.

• Mpaka kifo chake, AKA alikuwa na miaka 35.

Rapa wa Afrika Kusini, AKA
Rapa wa Afrika Kusini, AKA
Image: Instagram

Msanii AKA kutoka Afrika Kusini ameripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi muda mfupi baada ya kushuka kutoka kwa gari lake katika barabara moja kwenye taifa hilo lenye watu wa kila rangi, kusini mwa bara la Afrika.

Kulingana na taarifa kutoka kwa vyombo vya habari vya nchi hiyo, AKA mwenye umri wa miaka 35 alifariki baada ya watu wasiojulikana kumvizia na kummiminia risasi Ijumaa jioni alipokuwa akielekea katika sehemu moja ya burudani kutumbuiza.

Alikuwa ameshuka kwenye gari lake wakiwa na mtu mwingine na muda mfupi baada ya kusimama kwenye ukuta wa mgahawa mmoja wakijitayarisha kuingia ndani ili kutumbuiza, mtu asiyejulikana aliwaelekezea mtutu wa bunduki na kuwaua papo hapo, jarida moja liliripoti.

Taarifa za ndani zimeeleza kuwa wawili hao walipigwa risasi saa mbili usiku kwa saa za huko na kwamba magari mawili yalipita huku abiria wakifyatua risasi kwa mfululizo.

AKA ambaye jina halisi ni Kiernan Jarryd Forbes alikuwa anatarajiwa kutumbuiza katika kilabu cha usiku kiitwacho YUGO lakini hafla hiyo ilighairishwa na taarifa kwenye mitandao ya kijamii ikisema kuwa tamasha hilo lilikuwa likiachwa "kwa sababu ya hali zisizoweza kuepukika", Times Live waliripoti.

Taarifa za madaktari wa dharura zilidai kuwa rapa AKA alipatwa na risasi mara sita mwilini mwake na kwamba wakati wanapewa huduma ya kwanza, hakuwa anaonesha dalii zozote za uhai.

Rapa huyo ana umaarufu mkubwa kote ulimwenguni lakini katika ukanda wa Afrika Mashariki wengi watamshukuru msanii namba moja wa muda wote Diamond Platnumz kwa kufanya collabo naye mwaka 2016, ngoma iliyokwenda kwa jina ‘Make Me Sing’

Wimbo huo ulifanya vizuri sana kwenye chati za muziki kote Afrika Kusini na ukanda wa Afrika Mashariki na miaka 6 baadae, unajivunia watazamaji Zaidi ya milioni 13 kwenye mtandao wa YouTube.

Katika wimbo huo uliowafanya wengi wa mashabiki kutoka Afrika Mashariki kumjua AKA, maudhui yake mwanzoni yanaanza tu jinsi ambavyo alipatana na umauti wake – watu wenye silaha kali wanaonekana kulivamia jumba moja kabla ya kufanya uvamizi, na kutoroka na mali.

Matukio ya watu maarufu kuvamiwa kwa njia hiyo nchini Afrika Kusini si mageni kwani kwenye mitandao ya kijamii, wengi waliomuomboleza AKA waliibua kumbukumbu kuwa njia kama hiyo ndiyo msanii nguli wa miziki ya Reggae Lucky Dube alipatana na umauti wake miaka kadhaa iliyopita.