Solomon Mkubwa afichua mchango wa rais Ruto katika safari yake ya muziki kutoka 2013

Mkubwa alisema Ruto alishikilia nyimbo zake "Mfalme wa Amani" na " Mungu mweney nguvu" kipindi cha usinduzi wa Jubilee.

Muhtasari

• Msanii huyo alikiri kuwa baada ya kutumbuiza kwenye hafla hiyo ya 2013, ndio umaarufu wake ulienea kote nchini kila mtu akitaka kusikiliza nyimbo zake.

Solomon Mkubwa asimulia jinsi Ruto alimpa mafanikio katika miziki yake
Solomon Mkubwa asimulia jinsi Ruto alimpa mafanikio katika miziki yake
Image: Instagram, Facebook

Msanii wa injili Solomon Mkubwa amezungumzwa mara ya kwanza ambapo uhusiano wake mzuri na rais William Ruto ulianzia na jinsi kiongozi huyo alichangia mafanikio makubwa ya wimbo wake ‘Mfalme wa Amani’

Kinyume na watu wengi wanaojua kuwa uhusiano mzuri kati ya Mkubwa na Ruto ulianza katika kampeni za mwana 2022, Mkubwa alifichua kwamba wana miaka 10 tangu kujuana na rais Ruto.

Alisimulia kuwa Ruto kipindi hicho akiwa mbunge wa Eldoret Kaskazini alimfuata na kutaka kufanya kazi naye. Mwaka 2013 wakati Jubilee wanazindua manifesto yao, Ruto akiwa kama mgombea mwenza wa Uhuru Kenyatta katika tikiti ya mbio za kumrithi hayati Mwai Kibaki kama rais, Mkubwa aliitwa na Ruto ili kutumbuiza kwenye hafla hiyo.

“Rais alinikaribisha 2013 katika mkutano wa kuzindua manifesto ya Jubilee. Na kutoka wakati ule unajua rais ana ushawishi mkubwa sana kiasi kwamba akishikilia wimbo wako unakubaliwa na wengi. Alikuwa ameshikilia nyimbo zangu ‘Mfalme wa Amani’ na ‘Mungu Mwenye Nguvu’ na siku hiyo nilitumbuiza na Solomon Mkubwa akaenea Kenya nzima,” alisema.

Mkubwa alisema kuwa mpaka sasa uhusiano wake uko vizuri na ikitokea rais William Ruto amemtwika jukumu Fulani serikalini hawezi kufikiria mara mbili.

“Siwezi kata kwa sababu kila kazi kuna kuelekezwa, ukielekezwa unaenda kufanya kazi kwa ajili ya taifa.Nikipata kazi ambayo itakuwa inanipeleka kwa huduma yangu itakuwa vizuri sana,” Mkubwa alisema.

Awali aliwaombea wasanii wa injili msamaha baada ya Eric Omondi kuwatumbua kuwa ndio wanaoongoza katika matendo yasiyofurahisha katika jamii.