Msanii DNA azidiwa na hisia akikumbuka jinsi mtoto wake alikufa akiwa shuleni

"Jamal alifariki baada ya kuzama katika bwawa la shule,” DNA alieleza baina ya majonzi.

Muhtasari

• "Baada ya kumpoteza Jamal, kidogo tu niwapoteze watoto wengine kutokana na kuzama kwenye lindi la mawazo,” - DNA.

• “Ilinipiga vibya sana. Unajua mtoto wangu alikuwa ndio kila kitu." alisema.

Msanii DNA akumbuka jinsi mtoto wake alifariki.
Msanii DNA akumbuka jinsi mtoto wake alifariki.
Image: Facebok, Screengrab

Hakuna mzazi anayepaswa kumpoteza mtoto wake, kwa njia yoyote ile. Waliopigwa na bahati mbaya ya kuwapoteza watoto wao watakuhadithia kwa uchungu kuwa kwa mzazi, kumzika mtoto wako ni sawa na kuzika sehemu ya nafsi yako!

Kwa msanii DNA, hali haikuwa tofauti kipindi alimpoteza mtoto wake wa kiume kwa jina Jamal miaka kadhaa iliyopita.

Kwa simanzi na majonzi mazito, DNA alikumbuka mazingira ambayo yalisababisha kifo cha mtoto wake ambaye alimtaja kuwa “alikuwa kila kitu kwangu”

Msanii huyo mkongwe alisema hapendi kabisa kukumbuka tukio hilo kwani linaibua jeraha jipya kwenye moyo wake kwani hajawahi pona kutokana na mshtuko huo.

“Kusema kweli huwa sipendi kuzungumzia kuhusu mtoto wangu Jamal na jinsi yote yalitokea, kwa sababu huwa inanitupa katika kina kirefu sana cha mawazo. Juzi nilimuona mamake Jamal na ilinipa Amani ya nafsi kwamba hakuna mmoja kati yetu angeweza kurekebisha kilichokuwa tayari kimetokea. Jamal alifariki baada ya kuzama katika bwawa la shule,” DNA alieleza baina ya majonzi.

Msanii huyo alisema kwamba tukio hilo lilimpiga vibaya sana kwani ni moja kati ya matukio “yasiyo ya kawaida” ambayo yalimtupa kwenye lindi la mawazo kwa muda mrefu wa maombolezo mpaka nusra kuwapoteza watoto wengine.

“Ilinipiga vibya sana. Unajua mtoto wangu alikuwa ndio kila kitu. Kuna vitu visivyo vya kawaida kama kumpoteza mtoto ambaye hakuwa mgonjwa. Baada ya kumpoteza Jamal, kidogo tu niwapoteze watoto wengine kutokana na kuzama kwenye lindi la mawazo,” DNA aliguna kwa uchungu mwingi kwenye sauti yake.