Chris Brown ampokonya mrembo simu na kuitupa mbali wakiwa jukwaani (Video)

Mrembo huyo alionekana kutomzingatia Brown ambaye alimualika jukwaani na badala yake kukita macho kwenye simu yake.

Muhtasari

• Brown si mgeni kwa sintofahamu na utata kwani mwezi jana alionesha hasira yake hadharani baada ya kupoteza Grammy.

Chris Brown amejipata katika jungu la mjadala mkali mitandaoni baada ya kuonekana akimpokonya mwanadada simu yake kwenye jukwaa na kuitupa mbali kwenye umati wa waliohudhuria tamasha hilo.

Brown ambaye alikuwa anatumbuiza katika tamasha la "Take You Down." nchini Ujerumani na alimualika mwanadada huyo kwenye jukwaa na kumpa kiti kabla ya kuanza kucheza densi mbele yake umati ukishangilia.

Hata hivyo, mwanadada yule hakuonekana kuzingatia misakato ya Brown na badala yake alionekana muda wote kwenye simu yake akifanya kama kujirekodi video mwenyewe huku maskini Chris Brown akiendelea kujitutumua kando na mbele yake kwa staili mbalimbali za kunengua.

Mara ya kwanza, Brown aliichukua simu ya mwanadada yule kutoka mikononi mwake na kuiweka kwenye mapaja yake, ishara kwamab alikuwa anataka uzingatifu wote kwa asilimia mia kutoka kwa mrembo yule, lakini sikio la kufa halisikii dawa.

Mrembo yule tena alirudi kwenye simu yake na kuendelea kuiangalia akiipekua badala ya kutupa macho yake na uzingatifu kwa Brown.

Kitendo hiki kinatajwa kuwa kilimghasi Chris Brown ambaye kwa hasira aliichukua simu ile kwa kasi na kuitupa kwenye hadhara.

Mwanamke huyo aliyeonekana kukasirika kisha akarusha mikono yake hewani kabla ya taa za jukwaani kuzimwa na mpambano huo usio wa kawaida ukaisha.

Video hiyo ilisambaa haraka kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya mashabiki wakimtetea Brown huku wengine wakitaja kuwa ni mlipuko mwingine kutoka kwa mwimbaji huyo mwenye utata.

"Sikiliza, nakubali kabisa kwamba wakati mwingine sote tunahitaji kuwa na uwezo wa kuweka simu zetu chini na kufurahia wakati ... lakini hiyo si Chris Brown au uamuzi wa mtu mwingine yeyote kufanya," mtu mmoja alitweet.

"Haiwezekani kumtetea Chris Brown anaendelea kufanya mambo 😭," mwingine aliongeza kwa hasira.

Wengine, hata hivyo, walitetea kitendo chake, “Lowkey naona kwa nini Chris Brown alirusha simu. Unamaanisha tu niambie nitakuwa hapa nikiigiza moyo wangu, kukupa bora zaidi niliyopata na utakuwa hapa ukijiangalia kwenye kamera ya selfie. Kutokuheshimu?”

Brown, 33, sio mgeni linapokuja suala la kusababisha mabishano ya utata. Mwimbaji huyo wa "No Guidance" aligonga vichwa vya habari mwezi uliopita kwa kuwa na hasira baada ya kupoteza Grammy kwa Robert Glasper.