Mchekeshaji Vinnie Baite afichua chimbuko na maana ya jina lake "Baite"

Mcheshi huyo alisema ni jina linalotumiwa sana na Wameru, na linatamkwa kama "Baite" wala si "Vaite".

Muhtasari

• "Lazima ujue kitu unafanya ndio uitwe Baite,” Mchekeshaji huyo alisema.

• Mcheshi huyo alisema kwamba wanaolitamka kama "Vaite" ni wale wa nje ya Meru kwani huko jina hilo ni "Baite"

Mchekeshaji Vinnie Biate azungumzia chimbuko la jina lake
Mchekeshaji Vinnie Biate azungumzia chimbuko la jina lake
Image: Facebook

Mchekeshaji Vinnie Baite kutoka Meru kwa mara ya kwanza amefafanua kuhusu chimbuko na maana ya jina lake “Baite”

Baite alikuwa akizungumza kwenye podikasti moja ambayo kwa upana, alielezea kwamba jina Biate ni maarufu sana miongoni mwa jamii ya Ameru, ambalo mtu yeyote ambaye anaonekana kujua kitu anachokifanya huitwa aghalabu.

“Baite inamaanisha tu mwanamume ambaye anajua kitu anafanya, lakini si lazima uwe Mmeru, ukienda Meru mtu tu anaweza kuita Baite. Lazima ujue kitu unafanya ndio uitwe Baite,” Mchekeshaji huyo alisema.

Alikanusha kuwa jina hilo halitamkwi kama “Vaite” kama ambavyo watu wengi wanalitamka ama kulijua.

“Wanaoitamka kama ‘vaite’ ni wale ambao hawajawahi enda Meru, ukienda Meru hakuna kitu kama ‘vaite’ ni ‘baite’ na ndivyo hivyo linafaa kutamkwa,” Baite alisema.

Mcheshi huyo wa Meru pia hakukosa kuzungumzia Mirungi, au miraa kama ambavyo wengi wanaijua kwamba inapunguza nguvu za kiume kwa watumizi wake.

Alikanusha kwamba hiyo ni dhana tu ambayo imekuwa ikienezwa haswa na watu wanaojiita madaktari wa kienyeji wanaotaka kupata soko kwa dawa zao.

“Miraa ingekuwa inamaliza nguvu basi Wameru hawangekuwa na watoto, labda hata mimi nisingezaliwa kwa sababu mzee wangu alikuwa anatafuna sana. Kitu naweza kubali ni kwamba huwa inaharibu meno kwa rangi tu lakini si kuathiri,” Vinnie Baite alisema huku akicheka.