Bahati aahidi kufanya collabo ya pamoja na wasanii wote wa Meru, "Nitalipia kila kitu!"

Bahati alisema yuko tayari kurudisha mkono kwa jamii ya Ameru ambao wamekuwa wakimsapoti tangu alipoanza.

Muhtasari

• "Wasanii wangu wa Meru, hamuhitaji kwenda Nairobi ili kufaulu. Mnaweza kutimiza ndoto zetu kutoka sehemu yoyote mlipo,” Bahati alisema.

Bahati kushirikiana na wasanii wa meru kimuziki.
Bahati kushirikiana na wasanii wa meru kimuziki.
Image: Instagram

Msanii Kevin Bahati ameahidi kufanya collabo na wasanii wote wa kutoka Meru kama njia moja ya kuwainua wasanii hao ili pia kufikia viwango vya juu.

Akizungumza katika hafla ya msanii mwenza Jaysoul, wasanii wa Meru walimtaka kuwashika mkono na msanii huyo akawaahidi kuwa angependa kufanya collabo nao wote, ambapo pia alitoa ahadi ya kugharamia kila kitu katika collabo hiyo.

“Tunataka collabo mbili, Bahati tusaidie. Yako na pia ututafutie msanii mwingine,” msanii mmoja alisikika akimuomboa.

“Wacha niwaambie, hata tunaweza kufanya ya wasanii wote wa Meru, hakuna shida. Hakuna kitu kigumu kutimiza. Wasanii wangu wa Meru, hamuhitaji kwenda Nairobi ili kufaulu. Mnaweza kutimiza ndoto zetu kutoka sehemu yoyote mlipo,” Bahati alisema.

Hafla hiyo ya msanii Jaysoul ilihudhuriwa na wasanii wengine kama Nadia Mukami na Kenzo Matata huko Meru na Bahati alisema kwamba yuko radhi kurudisha mkono wake kwa jamii ya Ameru kama moja ya jamii ambazo zimekuwa zikimshikilia mkono katika safari yake ya muziki tangu alipoanza akiwa katika tasnia ya injili.

Alisema kwamba bado ameokoka na yeye kuacha kuimba injili haimaanishi kwamba alimuasi Mungu bali ni kazi tu ya kutafuta unga, huku akiwataka mashabiki wake wasikuwe wanachukulia kitu kwa umakini na kumtupia maneno kisa haimbi injili.