Wachungaji wa Bungoma waungana kumkemea Yesu wa Tongaren, "Ni njaa inamsumbua!"

"Hawa watu wote tumejitenga nao na hata hawajawahi kuja katika kanisa lolote na hatuwajui. Huyo mzee ni njaa inamsumbua."

Muhtasari

• “Watu wanaotaka kutumia vibaya majina ya Mungu, watu wanaosema kwamba wao ni Yehova Yesu wa Tongaren, tunakemea kwa jina la Yesu" - wachungjai hao walisema.

Wachungaji Bungoma wamkemea Yesu wa Tongaren
Wachungaji Bungoma wamkemea Yesu wa Tongaren
Image: Screengrab// youtbe

Wachungaji katika kaunti ya Bungoma wameungana na kuzungumza kwa sauti moja dhidi ya Yesu wa Tongaren, mwanamume anayejiita kuwa Yesu mwana wa Mungu ambaye ametumwa kuja kuukomboa ulimwengu.

Katika video moja ambayo imepakiwa mitandaoni, wachungaji hao wengi ambao nyuso zao zilionekana kuwa na ghadhabu walitoa tamko kali wakisema kwamba watu ambao wanazunguka wakijitapa kuwa Yesu wa Biblia ni waongo ambao wanatumia fursa kuwarubuni waumini wa Kikristo.

“Watu wanaotaka kutumia vibaya majina ya Mungu, watu wanaosema kwamba wao ni Yehova Yesu wa Tongaren, tunakemea kwa jina la Yesu. Tumekutana pia kujitenga kiudhabiti kabisa na mambo ambayo mmekuwa mkisikia katika vyombo vya habari ya kwamba kuna Yesu wa Tongaren, kuna Jehova Wanyonyi, kuna Yohana Mbatizaji, huo ni upotovu mkubwa wa kukosa ufahamu wa Biblia,” mchungaji mmoja alisema.

Wachungaji hao walikejeli Yesu wa Tongaren kwa dhana kwamba hakuna binadamu yeyote anaweza kuwa Yesu. Waliomba walimwengu wote ambao walisikia upotovu huo na kuwataka kuwa na Imani kwamba ni uongo wala si Yesu anayesimuliwa kwenye kurasa nyingi za Biblia Takatifu.

“Ni watu kutokuelewa Bilbia, kujiita eti ni Yesu wa Tongaren, hakuna kitu kama hicho kabisa. Hawa watu wote tumejitenga nao na hata hawajawahi kuja katika kanisa lolote na hatuwajui. Huyo mzee ni njaa inamsumbua,” walisema.

Walisema kwamba Yesu wa Tongaren ni ishara ya nyakati za mwisho ambazo zinasimuliwa katika Biblia kwamba watakuja watu waongo, yeye akiwa muongo wa kwanza kuonekana akilitumia jina la Yesu.