Mbunge Peter Salasya akiri kutatizika katika kujieleza kwa lugha ya Kiingereza

Salasya alitoa agizo kwashule zote za kutwa Mumias East kuanza kuzungumza Kiinereza muda wote, ili "wanafunzi wasije kuwa kama yeye"

Muhtasari

• Katika kuwasilisha hoja yake ya kwanza bungeni, Salasya alitatizika kujieleza kwa lugha ya kimombo, mara kwa mara akiradidi makosa ya kumrejelea naibu spika wa kike kama "bwana spika"

Mbunge Salasya asema mshahara hautoshi
Mbunge Salasya asema mshahara hautoshi
Image: Twitter

Mbunge wa Mumias ya Mashariki Peter Salasya amekiri kwa mara ya kwanza kwamba lugha ya wakoloni – Kizungu humpa changamoto sana katika kujieleza.

Mbunge huyo ambaye alikuwa katika ziara za shule za kutwa zilizopo kwenye eneo bunge lake kaunti ya Kaakmega alipakia mfululizo wa video akishangiliwa na wanafunzi katika shule hizo.

Alisema kwamba asingependa wanafunzi wa shule za kutwa kuwa kama yeye ambaye anatatizika kujieleza kwa Lugha ya Kimombo kwani enzi zake akiwa mwanafunzi, hawakuwa wanaambiwa umuhimu wa kujifunza kuzungumza au kuwasiliano kwa lugha hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Salasya alitoa amri kwa shule zote za kutwa kukumbatia mawasiliano kwa lugha ya Kimombo katika eneo bunge lake.

“Leo ni ziara za wapiga kura wa siku zijazo katika eneobunge langu....nimeagiza shule za kutwa za jimboni kwangu zitakuwa zinaongea Kingereza. Wasikuwe kama mimi Kizungu ‘si mdomo changu’. Mimi hutatizika kidogo kwa sababu sikuwa nazungumza Kiingereza,” Salasya alisema.

Mbunge huyo ambaye ndio mara yake ya kwanza kuchaguliwa katika wadhifa wa kisiasa pia alijitapa kuwa ni kipenzi cha wengi, si wadogo si wakubwa – wote wanamkubali pakubwa.

“Peter Salasya ni mnyama wa kijamii anayependwa na kila mtu ...huwezi kunichukia. ..na ninampenda kila mtu tu mtu mwenye kanuni sana wakati wa kushughulikia mambo mazito ya taifa,” alijigamba.

Mwaka jana baada ya kula kiapo bungeni na kuanza rasmi majukumu ya kuwatumikia wapiga kura wake, Salsya aligonga vichwa vya habari alipotatizika kujieleza kwa ufasaha kwa lugha ya Kimombo bungeni katika kuwasilisha kwa hoja yake ya kwanza kama mbunge.

Katika kikao hicho cha kwanza, naibu spika Gladys Shollei alikuwa anaongoza kikao hicho lakini Salasya aliradidi kumtambua kama ‘bwana spika’ licha ya kurekebishwa kwa safari nyingi kumrejelea kama ‘madam spika’.