Alikiba ashtushwa na uvumi kwamba ameshirikishwa kwenye albamu ya Davido, akanusha!

Hata hivyo, bosi huyo wa Kings Music alisema kwamba kufanya collabo na Davido ni jambo ambalo linawezekana.

Muhtasari

• "Inawezekana nifanye ngoma na Davido ndio maana watu wameeneza hilo, lakini kiuhalisia inafaa umuulize mtu" - alisema.

• Albamu mpya ya Davido inatarajiwa kutoka hivi karibuni.

Alikiba akanusha kufanya collabo na Diamond
Alikiba akanusha kufanya collabo na Diamond
Image: Alikiba//Instagram

Tangia Jumatano, kumekuwa na orodha ambayo ilikuwa inaenezwa mitandaoni ikionesha orodha ya ngoma za albamu mpya ijayo ya msanii nguli kutoka Nigeria, Davido.

Katika orodha hiyo ambayo haijulikani iliasisiwa na nani, ilikuwa ikiwaonesha wasanii mbali mbali ambao walipata nafasi ya kupewa shavu na Davido kwa maana ya Collabo, likiwemo jina la msanii kutoka Tanzania, Alikiba.

Mashabiki wa muziki haswa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki walifurika mitandaoni wakimsifia na kumhongera Alikiba kwa kuoata nafasi adimu ya kuwa kwenye albamu inayosubiriwa mno ya Davido.

Lakini sasa Alikiba mwenyewe amejitokeza wazi akipuuzilia mbali orodha hiyo inayomuonesha kuwa yuko miongoni mwa wasanii walioshirikishwa kwenye albamu ya Davido.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha habari nchini Tanzania, Alikiba alikanusha kufanya collabo na Davido na kusema kwamba hata kama kuna uwezekano wa kufanya collabo naye lakini hata siku moja hajawahi shirikiana naye kwenye wimbo, na hivyo kuzima uvumi huo.

“Kuna baadhi ya media ambao wanaweza wakakuza jambo bila kuwa na uhakika. Mimi sijawahi fanya wimbo na Davido. Inawezekana nifanye ngoma na Davido ndio maana watu wameeneza hilo, lakini kiuhalisia inafaa umuulize mtu. Nadhani sijaona kama Davido amepakia kitu kama hicho. Ni vitu ambavyo mimi mwenyewe vinanishangaza, mimi mwenyewe nimeshtuka kweli kweli, ni lini nilifanya wimbo na Davido?” Alikiba aliuliza.

Baada ya mfalme huyo kama anavyojiita kukanusha madai ya kufanya wimbo na Davido, inasalia kwamba Afrika Mashariki ni Diamond pekee aliyewahi kufanikiwa kuingia na Davido studioni.