Lazima tuwe na uwakilishi wa Bangi kwa Bipartisan - Jaymo Ule Msee

Jaymo ambaye aliongoza kampeni za Wajackoyah katika uchaguzi wa 2022 alisema pendekezo la kwanza liwe kupunguzwa kwa bei ya bangi

Muhtasari

• Ni lazima tuwe na uwakilishi katika timu ya mazungumzo hayo ya pande mbili,” Jaymo Ule Msee.

Jaymo Ule Msee ataka Waajckoyah kushirikishwa katika mazungumzo ya Bipartisan.
Jaymo Ule Msee ataka Waajckoyah kushirikishwa katika mazungumzo ya Bipartisan.
Image: Facebook

Aliyekuwa mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha kampeni za wakili msomi profesa George Wajackoyah, mcheshi Jaymo Ule Msee amemtaka Wajackoyah pia kushinikiza kujumuishwa katika maridhiano ya Bipartisan.

Mcheshi huyo kupitia ukurasa wake wa Facebook, alisema kuwa wafuasi wa Wajackoyah na chama cha Roots wana haki ya kujumuishwa katika mazungumzo hayo ya pande pindi ambayo yaliitishwa na rais Ruto wikendi iliyopita wakati alikuwa anamuomba Odinga kusitisha maandamano ili kupata mwafaka mezani.

Jaymo alisema kuwa moja ya ajenda kuu ambazo wawakilishi wao wanafaa kuzungumzia katika maridhiano hayo ni kupunguzwa kwa bei ya bangi.

“Wajackoyah pia apeane matakwa yake, bei ya bangi pia lazima iende chini. Ni lazima tuwe na uwakilishi katika timu ya mazungumzo hayo ya pande mbili,” Jaymo Ule Msee alisema.

Wikendi iliyopita, rais Ruto alimtaka kinara wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga kusitisha maandamano ili kutoa nafasi kwa mazungumzo ya pande mbili kuafikia mwafaka wa matakwa yao.

Odinga alikubali ombi hilo na kusitisha maandamano hayo makubwa ya Jumatatu ambayo alikuwa ameahidi kusimamisha shughuli zote jijini.

Baadhi ya matakwa ya mrengo wa upinzani kwa serikali ni kupungunzwa kwa gharama ya juu ya maisha, kusitisha mchakato wa kuteuliwa kwa makamishna wapya wa IEBC, kufunguliwa kwa seva za IEBC miongoni mwa matakwa mengine.