Bien: Kama mimi jina kubwa namepwa 14k, wale 'upcoming' kama Khaligraph watapewa ngapi?

Msanii huyo alikuwa anaonesha kiasi cha mirahaba ambayo MCSK imemlipa, kiasi ambacho baadhi walitaja ni mirabaha ya kati ya miaka 3 hadi 4.

Muhtasari

•Bien alishangaa kama yeye msanii anayetajwa kuwa namba moja amepokea kiasi hicho, wasanii chipukizi watapokea hela ngapi kama mirahaba.

Bien ashangaa kupokea 14k tu kutoka MCSK kama mirabaha
Bien ashangaa kupokea 14k tu kutoka MCSK kama mirabaha
Image: Instagram

Msanii Bien kutoka bendi ya Sauti Sol pia ameonekana kulalamika kuhusu malipo duni ya mirabaha ya kazi za wasanii kutoka MCSK.

Bien ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiongoza bendi ya Sauti Sol kufana kwenye muziki, huku wakiwa ndio wasanii pekee wenye takwimu kubwa kwenye majukwaa ya kidijitali ya kupakuwa miziki, alionekana kutupa dongo kwa MCSK akionesha kiasi kidogo cha fedha ambazo alipokea.

Katika ujumbe wa MPesa ambao alionesha Instagram, Bien alitumiwa shilingi 14,634 kutoka MCSK.

Akiandika ujumbe wa kinaya, Bien alijitaja kuwa ndiye msanii ambaye amepokea kiasi kikubwa kutoka MCSK na kusema ni tajiri mkubwa kwa wikendi hii huku akiwataka watu wajitokeze ili waungane naye katika kulimega bata.

Wakati huo huo pia aliwatania wasanii wenzake kama Khaligraph Jones akiuliza kama yeye jina kubwa amepokea kiasi hicho, kina Jones ambaye ni chipukizi atakuwa anapokea kiasi kipi.

“Wacha wikendi ianze. MIMI NI TAJIRI MTU!!!!! Majembe yapo wapi. Tunapiga sherehe bila udhibiti wikendi hii. Msanii wako nambari 1 amelipwa mrabaha. Ninaweza kufikiria wasanii chipukizi kama @khaligraph_jones wanapata nini. DM na mpango wa leo,” Bien alitania.

Bien si msanii pekee kulalamikia kuhusu mapato hayo. Msanii Harry Richie aliyefana kwa kibao Vaida pia alilalamika kupokea kiasi cha elfu 3 baada ya miaka mitatu na kusema kuwa kwa fedheha hiyo, ameamua kuacha muziki kabisa na kurudi kwenye kazi yake ya kitaaluma.

Wasanii wamekuwa wakilalamikia kupokea mirahaba ya kudunishwa kutoka MCSK kwa muda mrefu huku vilio na wito wao kwa serikali kutatua suala hilo katika Sanaa ukiwa unaanguka kwenye masikio yaliyotiwa pamba muda wote.