Msanii Harry Richie wa Vaida atangaza kuacha muziki baada ya malipo duni kutoka MCSK

"Narudi kwenye kazi yangu ya taaluma. Baki na miziki yenu,” Harry Richie aliandika baada ya MCSK kumtumia 3,228 pekee.

Muhtasari

• Richie aliambatanisha ujumbe huo na picha ya skrini ya miamala aliyopokea kutoka MCSK kupitia MPesa yake.

• Kulingana na picha hiyo, Richie alipokea shilingi 3228 kama mirabaha ya mapato ya ngoma yake ya Vaida.

 

Msanii wa vaida Harry Richie atangaza kuacha muziki.
Msanii wa vaida Harry Richie atangaza kuacha muziki.
Image: Harry Richie

Msanii wa nyimbo za injili aliyejizolea umaarufu kufuatia wimbo wake pendwa, Vaida, Harry Richie amekuwa msanii wa hivi punde Zaidi kulalamikia malipo duni ya mirabaha ya kazi za muziki kutoka kwa asasi ya kusimamia hakimiliki za kazi za wasanii nchini MCSK.

Richie kupitia ukurasa wake wa Facebook alilalamika kupokea mirabaha ya kiwango duni kutoka MCSK licha ya kudai kuwa wimbo wake, Vaida ulipata mapokezi makubwa na mafanikio kwa kiasi sawa.

Msanii huyo aliteta vikali akisema kuwa nchini Kenya kazi ya Sanaa haipati utambulisho unaofaa na kuwa msanii ni njia moja ya kujichimbia kaburi la umaskini, hivyo kusema kuwa rasmi ameacha muziki na kurudi katika kazi zake za awali.

“Kwa wale wanaoandika kuhusu sisi wasanii, jinsi tunavyoishi maisha ya kifahari. #Vaida imeisha lakini hii ndio tunalipwa mara mbili kwa mwaka. Kusema tu ukweli, mara ya mwisho nilipokea ujumbe kama huu ni 2020, Narudi kwenye kazi yangu ya taaluma. Baki na miziki yenu,” Harry Richie aliandika.

Richie aliambatanisha ujumbe huo na picha ya skrini ya miamala aliyopokea kutoka MCSK kupitia MPesa yake.

Kulingana na picha hiyo, Richie alipokea shilingi 3228 kama mirabaha ya mapato ya ngoma yake ya Vaida.

Harry Richie alalamika malipo duni ya MCSK.
Harry Richie alalamika malipo duni ya MCSK.

Awali, mwanamuziki ambaye pia ni mtangazaji Amani Aila alilalamika vikali baada ya kupokea shilingi mia sita na ushee, akisema kuwa ni vizuri mzazi wake alimsisitizia kusoma na kuacha muziki maana kwa pesa hizo hata jogoo wa kienyeji hawezi mudu kumnunua.

Karibu niwache shule sababu ya mziki,namshukuru marehemu babangu mzazi,alivyonikalia gangari.Ona sasa.... Kiasi cha chini cha kurekodi sauti ya wimbo mmoja -10,000, kiasi cha chini cha video ni 20,000 lakini mirabaha ya MCSK kwa miaka mitatu hadi minne ni 637 peke yake!” Aila alilalamika.